WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amekutana na Kikosikazi cha Miji Salama kinachoratibu na kusimamia utekelezaji wa mradi wa ufungaji wa kamera za kuzuia uhalifu.
Kamera hizo awali zitafungwa katika majiji matano ili kudhibiti matukio ya uhalifu ukiwemo ujambazi, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, wizi na matukio mengine ya kiuhalifu.
Majiji yatakayofungwa kamera hizo ni Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha huku lengo likiwa ni kufunga kamera hizo katika mikoa yote nchini kwa siku zijazo. Masauni alisema kuna maeneo ambayo yanatakiwa yawe na udhibiti wa uhalifu hasa kwa kutumia teknolojia na baadhi ya nchi tayari wana mfumo huo na wameanza kufanikiwa kudhibiti uhalifu na makosa ya ukiukwaji wa sheria za usalama.
“Serikali tumeanza jitihada za kufunga kamera, sasa mkiwa wajumbe wa kikosi kazi mfahamu mna jukumu kubwa kwa nchi kuhakikisha mradi huu unatekelezeka ili uwe na manufaa kwa nchi yetu,” alisema. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Camilius Wambura aliagiza wajumbe wa kikosikazi hicho wahakikishe wanaupitia mkataba huo wa ufungaji wa kamera hizo.
No comments:
Post a Comment