Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Salum Morcase amkamate Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Saad Ishabailu kwa kosa la kuhamisha shilingi milioni 213.74 akishirikiana na watumishi wa TAMISEMI na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.
Ametoa agizo hilo Februari 27, 2024 wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenye kikao kilichofanyika kwenye Halmashauri hiyo, mkoani Mara ambapo Ishabailu anadaiwa kufanya uhamisho kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho wa ndani.
“Mkamate huyo bwana sasa hivi aende polisi akafunguliwe
mashtaka, huyu ni wa kupeleka mahakamani moja kwa moja. DPP aelezwe afungue jalada la mashtaka. Wale wenzake tumewapeleka
mahakamani tayari sababu tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa
ya Kigoma mwaka jana, ” ameagiza Waziri Mkuu.
Amesema Juni 21, mwaka jana
Ishabailu alianza kufanya matumizi ya hizo fedha kwa kushirikiana na
mfanyabiashara wa Mugumu, Daudi Matinde Chacha kupitia kwenye akaunti zake za
NMB na CRDB kwa kupitia miamala minne ya shilingi milioni 76.3, milioni 57.7,
milioni 47 na shilingi milioni 32.5.
Ameongeza kuwa alipoulizwa na timu ya uchunguzi Matinde alikiri kuwa haidai fedha yoyote Halmashauri ya Serengeti isipokuwa Mweka Hazina huyo aliomba apitishie fedha zake kwenye akaunti zake kwa sababu zinahitajika haraka kwa matumizi ya ofisi.
“Aliambiwa atoe shilingi milioni 189 akamkabidhi zote Ishabailu na zilizobakia (shilingi milioni 24) akaambiwa abaki nazo,” amesema Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasisitiza madiwani na watumishi kuwa
makini na matumizi ya fedha za umma kwani Rais Samia Suluhu Hassan anatafuta
fedha na kuzileta kwenye Halmashauri ili zije kutatua kero za wananchi.
Chanzo : Global Publishers
No comments:
Post a Comment