Serikali imedhamiria kuyafanya makazi ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyoko kijiji cha Mwitongo, wilayani Butiama mkoani Mara kuwa kituo cha utalii.
Waziri Mkuu Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Moses Kaegele atembelee eneo, akagua na kuangalia mapungufu yaliyopo ili Serikali iweze kuyafanyia kazi. Pia ameiagiza wizara ya ujenzi ishughulikie barabara ya kutoka Serengeti hadi Butiama ili ikamilike na kuwawezesha watalii wanaotaka kufika kwenye makumbusho hayo kwa njia ya barabara.
Waziri Mkuu alipitia Mwitongo na kuwasalimia wanafamilia wa Baba wa Taifa na kuweka shada la maua kwenye kaburi lake.
Mapema, alipowasili
wilayani humo, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa
Wilaya ya Butiama ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 60.
Akizungumza mara
baada ya kuweka jiwe hilo, Waziri Mkuu alimtaka mkandarasi wa mradi huo ambaye
ni Wakala wa Majengo (TBA) ahakikishe anaukamilisha mradi huo kwa wakati. Hadi
sasa, mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 843.4 ikiwa ni malipo ya awali na hati
za malipo ya pili na tatu.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) inaendelea na kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji ambapo kazi kubwa
imefanyika na sasa nguvu kubwa inaelekezwa kwenye kufikisha umeme kwenye vitongoji.
Akizungumza
na wakazi wa Issenyi, wilayani Serengeti, akiwa njiani kuelekea Mugumu,
Mheshimiwa Majaliwa alitoa rai kwa Watanzania waachane na matumizi ya kuni na
mkaa na badala yake waanze kutumia gesi.
Chanzo : FullShangwe
No comments:
Post a Comment