Baada ya uhai wake kuisha, ukanda maalumu wa kiuchumi (SEZ) katika eneo hilo unatajwa kuanzishwa kama mbadala wa mgodi huo.
Mgodi wa Buzwagi ulikuwa wa pili kwa ukubwa nchini, ukiwa umeajiri watu zaidi ya 3,000. Ulifungwa rasmi Julai 2022.
Katika kuanza kutekeleza hilo, kampuni ya dhahabu Barrick ambayo ilikuwa inamiliki mgodi huo imeanza urejeshaji wa mazingira ya mgodi katika hali yake au iliyo bora zaidi kama utaratibu unavyotaka.
“Mgodi umefungwa lakini tunaendelea kurudisha eneo lile katika hali yake, ufukiaji wa mashimo umekamilika, utoaji maji kwenye makaro unaendelea, ufukiaji wa madimbwi unaendelea,” amesema Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow.
Amesema kwa sasa shughuli inayoendelea ni kurudisha eneo hilo la mgodi katika hali ya kawaida au iliyo bora zaidi, lakini pia kutekeleza miradi inayochagiza maendeleo katika maeneo tofauti.
Bristow amesema katika kufanya hivyo, Barrick wamejenga jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Kahama jirani na ulipokuwa mgodi huo, ambalo lina uwezo wa kuhudumia abiria 250 kwa wakati mmoja. Lililokuwapo awali lilihudumia watu 25.
Amesema kampuni hiyo itaendelea kufanya uchimbaji endelevu kwa ajili ya kutengeneza thamani kwa wadau na kuhakikisha inaacha urithi mzuri unaoendelea kuhudumia jamii kwa muda mrefu, baada ya uchimbaji kufika mwisho.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, licha ya kuahidi mkoa kuendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni za Barrick na Twiga, amemuomba mkuu wa kampuni kueleza maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Tanzania ili kuvutia uwekezaji zaidi kutoka nje.
Bristow akizungumzia ombi hilo, amesema jambo la muhimu na kubwa ni kuimarisha shughuli za usafirishaji na uchukuzi kwa kuwa na bandari yenye ufanisi mzuri na mtandao wa reli na barabara, unaounganisha maeneo muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mdeme akielezea mradi wa ukanda maalumu wa kiuchumi wa Buzwagi, amesema ana imani utaleta manufaa kwa wananchi wa Kahama ikizingatiwa kuna miradi mingi inaendelea nchini, ambayo italifanya eneo hilo kuwa la kimkakati.
“Tunataka kuweka mzunguko wa kiuchumi katika eneo lile kama ilivyokuwa, tutakuwa na bandari kavu katika eneo lile, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) maboresho yanayofanyika bandarini huko na ujenzi wa eneo maalumu la kiuchumi kutapachangamsha sana,” amesema.
Ameiomba Wizara ya Madini kutoa maelekezo kwa kampuni zote za madini kuwa na utaratibu kufanya kikao cha pamoja na viongozi wa Serikali, wananchi na wadau wote wa sekta hiyo ili kutoa mrejesho wa yale yanayojiri.
SomaZaidi:https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/eneo-la-kiuchumi-laanzishwa-kahama-kama-mbadala-wa-mgodi-wa-buzwagi-4500232
No comments:
Post a Comment