MATOKEO KIDATO CHA NNE BADO NI CHANGAMOTO GEITA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 30 January 2024

MATOKEO KIDATO CHA NNE BADO NI CHANGAMOTO GEITA

Licha ya ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne mkoani Geita mwaka 2023 kuongezeka kwa asilimia 4.1, takwimu zinaonyesha asilimia 62.2 ya wanafunzi hao wamepata daraja la nne na sifuri.

Wanafunzi 18,274 walifanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2023 kati yao wavulana walikuwa 9,500 na wasichana 8,774, huku waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ni wanafunzi 6,868 sawa na asilimia 37.5.

Katika matokeo hayo, wavulana wamefanya vizuri ikilinganishwa na wasichana ambapo kati ya wavulana 9,500 waliohitumu 4,635 sawa na asilimia 48.7 wamepata daraja la kwanza hadi la tatu, huku wasichana 2,233 sawa na asilimia 25.4 wakipata madaraja kama hayo.

Pia kati ya wasichana 8,774 waliohitimu, 6,542 sawa na asilimia 74.5 wamepata daraja la nne na sifuri.

Ofisa Elimu Mkoa wa Geita, Antony Mtweve akizungumza na Mwananchi Digatal jana Jumatatu Januari 29, 2024 amesema wamefaulisha wanafunzi kwa asilimia 90.1 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.1 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana ambayo ufaulu ulikuwa asilimia 85.9.

Amesema kati ya shule 141 zilizofanya mtihani huo, shule 32 zikiwepo za Serikali 15 zimefuta sifuri na kwamba mafanikio hayo yametokana na uboreshwaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyopunguza msongamano darasani pamoja na ujenzi wa mabweni kwa baadhi ya shule.

Mmoja wa wadau wa elimu mkoani Geita, Bernadetha Obuya ambae pia ni Meneja wa Shule ya Sekondari ya Geita Adventist, amesema motisha kwa walimu na nidhamu kwa wanafunzi ni moja ya mambo yaliyochangia kuongeza ufaulu.

Katika shule hiyo, amesema wanafunzi 231 walihitimu na kati yao 181 wamepata daraja la kwanza, 50 daraja la pili na kwamba siri ya mafanikio hayo ni ushirikiano uliopo kati ya uongozi wa shule na walimu, utoaji wa motisha kwa walimu, nidhamu kwa wanafunzi na kumtanguliza Mungu kwenye kila kitu.

“Mwalimu akipenda kazi yake mtoto atafanya vizuri, ukishajenga mazingira mazuri na ukawaheshimu hakuna mwalimu mbaya,” amesema Obuya.

Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo, Themistocles Chrizoston amesema ili kupunguza tatizo la wanafunzi kufanya vibaya hasa kwenye somo la hesabu, walimu wanapaswa kuwasaidia na kuwapa muda wa kutosha wa kufanya somo hilo wenyewe mara kwa mara na pindi wanapokwama mwalimu awasaidie ili wajiamini na kuliona ni somo la kawaida.

Amesema ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi nchini, Serikali inapaswa kuzingatia uwiano kati ya mwalimu na mwanafunzi ili aweze kuwafikia wanafunzi wote.

“Kama tunataka kuboresha elimu yetu tuangalie idadi ya wanafunzi na walimu waliopo, darasa walau liwe na wanafunzi wasiozidi 50 ili mwalimu apate muda wa kutosha wa kuwafikia wanafunzi wote,” amesema Chrizoston.

Janeth Elias, Mkazi wa Mtaa wa Mission Mjini Geita amesema bado juhudi zinahitajika kumuwezesha mtoto wa kike kufanya vizuri na kwamba ujenzi wa mabweni unaoendelea katika shule mbalimbali za Serikali utawasaidia wanafunzi hasa wanaotoka kwenye familia duni kupata muda wa kujisomea bila kukumbana na vishawishi.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso