Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kudhibiti rushwa unahitajika uongozi imara pamoja na kuishirikisha jamii na wadau kuanzia ngazi ya watoto shuleni.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akishiriki mjadala wa ngazi ya juu uliyohusu masuala ya Utawala Bora na kukabiliana na Rushwa uliyofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi.
Amesema rushwa imekua changamoto kubwa inayoleta madhara zikiwemo rushwa za ndani ya mataifa na zile za kimataifa.
Akitoa uzoefu wa Tanzania katika kupambana na rushwa, Makamu wa Rais amesema serikali imeweza kuendelea kufanikiwa kupunguza kiwango cha rushwa kwa kuimarisha taasisi za utawala kama vile ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kuhakikisha anawezeshwa kwa rasilimali fedha na rasilimaji watu, vifaa na uwezo wa kutumia teknolojia ili aweze kufutilia matumizi ya serikali.
Pia Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuwepo kwa mfumo wa uangalizi kutoka Bunge la Tanzania kupitia kamati za bunge kama vile Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambazo hufanya ufuatiliaji wa matumizi ya serikali.
Makamu wa Rais amesema kwa kuzingatia serikali hufanya manunuzi kwa asilimia kubwa, hivyo imeimarisha Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma ili kudhibiti rushwa katika michakato ya manunuzi.
Pia amesema nchini Tanzania wadau mbalimbali na watu binafsi hufanya ufuatiliaji wa matumizi ya serikali na mwenendo wa rushwa kwa kutumia taasisi binafsi.
Halikadhalika amesema ripoti mbalimbali kutoka kwa mashirika binafsi husaidia katika kutambua mwenendo wa vitendo vya rushwa na hivyo kuweka mikakati ya kukabiliana navyo.
Makamu wa Rais amesema kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia pamoja na uwazi katika michakato mbalimbali ya uwekezaji hususani katika sekta ya madini kumesaidia katika kupunguza vitendo vya rushwa.
Makamu wa Rais yupo nchini Uswisi ambapo anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa mjadala wa ngazi ya juu uliyohusu masuala ya Utawala Bora na kukabiliana na Rushwa uliyofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi. Tarehe 18 Januari 2024.
No comments:
Post a Comment