EU YAWEKA NGUVU MIRADI REA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 12 December 2023

EU YAWEKA NGUVU MIRADI REA



DAR ES SALAAM: SERIKALI imepokea magari 21 kati ya 29 yenye thamani ya Sh bilioni 1.9 kutoka ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).


Akizungumza wakati wa kupokea magari hayo leo katika ofisi ndogo za REA jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameishukuru EU kwa kuendelea kuisadia serikali katika miradi mbalimbali ikiwemo huu wa usambazaji wa nishati kwa wananchi vijijini.


“Hii sio mara ya kwanza Umoja wa Ulaya wametusaidia, wamekuwa wakitushika katika miradi mbalimbali ikiwemo Kituo cha kupoza umeme Ifakara (umeme wa kati 20MVA wenye kuzalisha Megawati 16),” amesema kiongozi huyo.


Naibu huyo pia ameiasa REA kutumia ipasavyo magari hayo ili kuhakikisha dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo inafikiwa.


Naye, muwakilishi wa Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Cedric Merej amesema ni fahari kwao kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu utakaoleta tija kwa wananchi wa vijijini.


“EU tunaamini msaada huu utagusa asilimia 30 ya wananchi wa vijijini jambo ambalo ni matokeo chanya na makubwa tunayoyatarajia.” Amesema Merej.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy amesema watahakikisha wanayatunza vizuri na kusimamia matumizi sahihi ya magari hayo ikiwa ni moja wapo ya mradi kati ya miradi kadhaa iliyokwisha kutekelezwa.


“Wamechangia utekelezaji wa miradi mikubwa minne. Kuna mradi wa kupeleka umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza. Pia wamechangia mradi wa ujazilizi awamu ya pili A.” Amesema Mkurugenzi huyo.


Amesema EU pia kwa kushirikiana na Serikali wanatekeleza miradi ya umeme inayoendelea maeneo ya Ifakara, Ulanga na Mvomero, pia mikakati ya Serikali ni kuhakikisha taifa linahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Chanzo: habarileo

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso