AFISAELIMU KATA YA KANYIGO WILAYANI MISSENYI, AWAHIMIZA JAMII KUSAIDIA ELIMU,AWAFAGILIA UMOJA WA HISA ENDELEVU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 3 December 2023

AFISAELIMU KATA YA KANYIGO WILAYANI MISSENYI, AWAHIMIZA JAMII KUSAIDIA ELIMU,AWAFAGILIA UMOJA WA HISA ENDELEVU

Afisaelimu wa Kata ya Kanyigo, wilayani Missenyi, Muchunguzi Ishabairu, amewahimiza wanajamii ambao wamejaliwa kuwa na uwezo wa hali na mali, kusaidia katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika kuinua taaluma ya wanafunzi katani humo.

Wanafuzi na wazazi/walezi wao wakifurahia msaada huo ( picha zote na Mutayoba Arbogast)

Na Mutayoba Arbogast, HUHESO DIGITAL Bukoba


Afisaelimu huyo ameyasema hayo mwishoni mwa wiki katika hafla ya utoaji wa misaada kwa wanafunzi 100 wa shule za msingi za Kigarama, Nshumba na Kanyigo katani humo, msaada uliotolewa na Kikundi cha Umoja wa hisa endelevu Kanyigo(UHIKA).


Afisaelimu huyo amesema, wapo watu wakubwa wenye uwezo wao kifedha, lakini hawafikirii kabisa kuwasaidia wahitaji, na akashauri kikundi cha UHIKA, kiwe chachu ya kuwafanya wengine kuiga mfano huo kuisaidia jamii.


"Kama ilivyo kauli mbiu yao, 'Kwa pamoja tunaweza' basi sote tushirikiane katika kuhakikisha watoto wetu wanapata mazingira bora ya elimu'', amesema Ishabairu.


Msaada huo wenye thamani ya sh 700,000 ni wa madaftari na kalamu za wino.


Mwenyekiti wa kikundi hicho, Theonesti Kashunja,amesema wao ni kikundi kidogo chenye wanachama 11, kimesajiliwa na halmashauri ya wilaya ya Missenyi kama kikundi cha kijamii, kikijihusisha na kukodi nyumba ya wageni katani humo iitwayo Mikimba Galaxy, ambapo kiasi cha faida inayopatikana huelekezwa katika kuisaidia jamii, na kuwa wataendelea kutoa kadri watakavyojaliwa, hasa kwa wanafunzi.


Licha ya msaada huo wa vifaa vya shule, Kikundi hicho kimeahidi kumlipia mwalimu wa kujitolea katika shule ya msingi Kigarama, shilingi  laki moja kila mwezi kwa miezi sita, kuanzia Januari 2024.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kigarama, Evodius Protace ameshukuru kwa msaada huo, huku akiuomba umoja huo na wadau wengine wa maendeleo, kuwasaidia kompyuta shuleni akisema sasa ni kipindi cha Teknolojia.

Wanafunzi na wazazi baada ya kupewa msaada katika picha ya pamoja


Mwanafunzi wa darasa la tatu, shule ya msingi Nshumba, Johaness Mwesiga, kwa niaba ya wenzake ameshukuru kwa msaada huo na kuahidi watautumia vizuri, huku akiomba wawatembelee tena kuwakagua na kujionea maendeleo yao.


Naye Afisa mtendaji wa Kata Kanyigo, Daud Kyaka, akasema wengine wanaweza kuona msaada huo ni kidogo, kumbe ni msaada mkubwa sana kwa jamii, ukizingatia hali ya watoaji msaada huo, kwani hawapati faida kubwa ila wamezingatia kujinyima kwa ajili ya jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso