Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewataka watafiti na wanavyuo nchini kutambua kuwa wanawajibu wa kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.
Katibu Mkuu amesema hayo wakati akifungua zoezi la utoaji wa zawadi kwa Wanachuo, Watafiti na Viongozi wa Chuo waliofanya vizuri kwenye masomo yao kupitia Ndaki mbalimbali za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) iliyofanyika chuoni hapo.
Prof. Nombo amesema Chuo ni sawa na Kiwanda kama Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyesema, Chuo ni kama Kiwanda kwa sababu kinazalisha wataalamu wanaopaswa kutumia utaalamu wao kwa manufaa ya jamii na kiwanda hicho kinapaswa kuzalisha wataalamu na wahitimu watakaokuwa na manufaa kwenye jamii na kuonesha umaana wa elimu na bila kutatua changamoto hakutakuwa na umaana wa elimu mtu aliyosomea.
“Ukisoma tu kama hutatua tatizo kwenye jamii umaana wa elimu yako unakuwa haupo, huo ni wito kwa watafiti na wahitimu wote waliopo kwenye vyuo watambue kuwa wanawajibu wa kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii” alisema Prof Nombo.
Alisema majukumu ya Vyuo Vikuu ni kufundisha, kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kuzifikia jamii na kwamba kwa kupitia matokeo ya tafiti ndipo jamii itafikiwa na kuchukua suluhisho la changamoto za kijamii zilizopo.
Naye mmoja wa watafiti aliyepata tuzo ya mtafiti bora wa mwaka kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya, Profesa Robinson Mdegela amesema amefanikiwa kupata tuzo hiyo baada ya kufanya tafiti yenye kugusa maisha ya Watanzania ikiwemo kupambana na ongezeko la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa tatizo linalokaribia kuua watu karibu 12500 kwa mwaka kiwango ambacho ni karibu mara 10 ya idadi inayosababishwa na malaria au UKIMWI.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema kwa mwaka huu 2023 wamefanikiwa kutoa zawadi 248 ambazo hutolewa kila mwaka ili kuonesha ushindani na kuleta mabadiliko makubwa.
Prof. Chibunda amesema mabinti wanaonekana kuwa mstari wa mbele katika kupata zawadi na kuongezeka kila mwaka jambo ambalo linaashiria wanazidi kuongeza juhudi ya kusoma na kuweka changamoto kubwa kwa wanafunzi wa jinsia ya kiume.
Naye mwanafunzi aliyepata tuzo tatu ikiwemo ya mwanafunzi bora wa kike na pia mwanafunzi bora mwaka wa tatu kwa Shahada ya Usimamizi wa Nyuki na Rasilimali Zake SUA Vaileth Chiwango alisema alipata tuzo hizo ambazo atazitumia kubadilisha jamii hasa inayofanya ufugaji wa nyuki kizamani kwa kutumia mizinga ya kisasa na kusimama kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment