Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga amewasihi wajumbe waliohudhulia katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi kwenda kutoa elimu kwa wazazi wa watoto wenye umri chini ya miaka 8 kuhakikisha wanajitokeza ili watoto wao waweze kupata huduma ya chanjo ya polio.
Na Mutayoba Arbogast, HUHESO DIGITAL, Bukoba
Akizunguza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya amesema kuwa elimu ikitolewa kwa wazazi na walezi wa watoto wataona umuhimu wa watoto wao kuchanja chanjo ya Polio ambayo itawalinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya Polio.
"Tusisite kuwambia tuwambie wananchi juu ya umuhimu na madhara ya kutochanja watoto chanjo ya polio" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Mkuu wa wilaya ya Muleba, Dr Abel Nyamahanga
Wilaya hiyo inatakiwa inakabiliwa na ugumu wa kijiografia kwani kati ya kata zake 43, kata tano ni za visiwani ndani ya ziwa Victoria, ambazo ni Goziba, Kerebe, Ikuza, Mazinga na Bumbire,ambazo ziko ndani ya visiwa 26 vyenye makazi ya watu,kati ya visiwa 38 vya wilaya hiyo, hivyo ni lazima zifikiwe.
Katika Tarifa iliyosomwa na Bi. Christina Mlemi ambaye ni Afisa chanjo wa wilaya hiyo, ameeleza kuwa ugonjwa wa pllio umeripotiwa katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa mnamo tarehe 29/06/2023 kwa mtoto wa umri wa mwaka mmoja na miezi 11 ambaye vipimo vyake vilipelekwa maabara na kutoa majibu chanya.
Hivyo, kutokana na mlipuko huo Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa tokomeza Polio waliamua kampeni hii ifanyike katika Mikoa sita ambayo inamuingiliano ambayo ni Kagera (watoto lengwa ni 729,387), Katavi (227,862), Kigoma (884,477), Rukwa (391,883), Mbeya (614,346), na Songwe (402,643).
Mlemi amemnukuu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akisema kuwa kuwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana nasi mfano Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia hivyo hali hii inaongeza tishio na hatari ya maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Polio kwa nchi yetu hususani katika Mikoa inayopakana moja kwa moja na nchi hizo.
“Napenda nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa tutakuwa na Kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Polio (nOPV2) kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane (8). Kampeni hii itafanyika kwa siku nne (4) kuanzia tarehe 21 – 24 Septemba, 2023 katika Mikoa sita (6) inayopakana na nchi zenye mlipuko wa Polio ambayo ni Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya” amesema Waziri Ummy.
“Lengo la kampeni hii ni kuwafikia watoto 3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili (Polio Virus Type 2) kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa ugonjwa wa Polio husababishwa na virusi vya polio ambavyo husababisha mtoto kulemaa na huingia mdomoni kwa njia ya kunywa maji au kwa njia ya kula vyakula ambavyo vimechafuliwa na kinyesi, mtoto asiyepata chanjo ya polio ni hatari katika maisha yake yote na jamii nzima kwa ujumla kwa sababu huambukizwa kutoka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mtoto mwingine.
Akizungumzia lengo la Kampeni ya Polio ni kuongeza uelewa kwa wanajamii kuhusu faida za chanjo ya Polio ambapo chanjo ya polio ndio kinga pekee ambayo inaweza kumlinda mtoto dhidi ya ugonjwa huo.
Kampeni hii itaanza rasmi kuanzia tarehe 21-24/09/2023 kwa ajili ya kuwalinda na kuwazuia watoto wote chini ya miaka 8 kuenea kwa virusi vya Polio na kupitia Kampeni hii Halmashauri ya wilaya ya Muleba inalenga kuwachanja jumla ya watoto laki 160,324.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Afya inatarajia kuendesha Kampeni ya uchanjaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto zaidi ya Milioni 3,250,598 walio chini ya miaka 8 katika mikoa tajwa.
Doricas Vicent, mzazi wa mtoto wa miaka miwili,mkazi wa Muleba mjini ameieleza Huheso Digital kuwa hajasikia habari juu ya chanjo hiyo ya polio, lakini kwa kuwa amepata habari hii,atajitokeza kumpeleka mtoto wake kuchanjwa,akisema hakuna mzazi asiyefurahia afya ya mwanawe.
Mugisha Rutagwerela (54), mkazi wa kata ya Kashenye wilaya ya Missenyi mkoani humo, ambaye ni mlemavu aliyepooza viungo akiwa mdogo kutokana na polio, amewahimiza wazazi wote na walezi wa watoto, kuitikia chanjo hiyo, kuwaepusha watoto na madhara na adha alizopitia kutokana na ugonjwa huo, ikiwemo kukosa fursa mbalimbali za maendeleo.
No comments:
Post a Comment