Jamii ya watu wenye ulemavu wa macho wameomba kusaidiwa Bima Maalum ya Afya ili kuwasaidia katika matibabu.
Mwenyekiti wa Chama cha wasioona (TLB) mkoani Manyara, Paulo Safari Akonaay amesema watu wengi wasioona wanaishi kama tegemezi kuanzia suala la kuoneshwa njia, chakula na malazi.
“Na utakuta watu tunaowategemea pia wana matatizo yao mbalimbali, hawawezi kutuhudumia kwa kila kitu,” amesema Akonaay, katika mkutano wa chama hicho uliofanyika wilayani Mbulu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa TLB, mara nyingi watu wenye uoni hafifu na matatizo ya macho ndio hupata matatizo makubwa zaidi katika changamoto za maisha na pia wao huwa vigumu zaidi kupata kazi au kufanya biashara.
“Nadhani pia tungewezeshwa ruzuku katika umoja wetu, tungeweza kuanzisha shughuli za kufanya ili kupunguza au kujiondoa kabisa kwenye masuala ya utegemezi,” Akonaay ameongeza.
Chama cha Wasioona, pia kimetoa ombi kwa jamii na serikali kuwasaidia wanachama wake kwa fimbo za kutembelea, kwa ajili ya usalama barabarani, kutengwe maeneo ya kuvukia na pia kupewa vifaa vya elimu na hata mafunzo mbalimbali.
Afisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Tomic Simbeye ambaye pia ni mlezi wa chama hicho amesema kwa sasa wanaendelea kutafuta wadau mbalimbali wa kuwasaidia watu hao kwa sababu serikali tayari ina majukumu mengi.
No comments:
Post a Comment