Bibi Beatrice Edward wa kijiji cha Mugongo, kata ya Ruzinga akihudumia shamba lake
MUTAYOBA ARBOGAST, HUHESO DIGITAL, BUKOBA
WAKULIMA wa zao la vanilla katika kata ya Ruzinga wilayani Missenyi, mkoa wa Kagera, wamemuomba Waziri wa kilimo, Hussein Bashe kuwasaidia mitaji mikubwa itakayowawezesha kuingia kwenye ukaushaji wa vanilla wenye tija na kufikia hatua za ukamuaji mafuta na kuuza matone kwa watengenezaji wa bidhaa itokanayo na vanilla.
Wakulima hao wameyasema hayo katani humo wakati mwandishi wa habari hii alipowatembelea hivi karibuni, kufuatilia namna wanavyosaidiwa na serikali hasa na wataalam wa kilimo na wadau wengine kuhakikisha zao hilo linawaletea nafuu ya maisha.
Shirika lisilo la kiserikali wilayani Missenyi,Shirika la Maendeleo na Matumaini Kanyigo (SMMK), kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) linaiwezesha Kamati ya Ufuatiliaji huduma katika kilimo hasa vanilla katika kupata matokeo chanya.
Vanilla ambayo haijakaushwa
Kwa mujibu wa takwimu toka Ofisi ya afisa kilimo wa kata hiyo, wakulima wa vanilla katani humo walizalisha tani 12.6 mwaka 2020, tani 10.4 mwaka 2021, tani 13.8 mwaka 2022 na tani 9.6 mwaka 2023,ikielezwa kuwa vanilla nyingine haikurekodiwa mwaka huu kutokana na kuharibikia shambani baada ya kukosa wanunuzi.
Kata hiyo mwaka 2023 imerekodi kuwa na wakulima 756 huku Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ikionesha kata hiyo kuwa na wakazi 1528.
Takwimu zaidi toka Ofisi hiyo ni kuwa bei ya kilo moja ya vanilla mbichi katani humo mwaka 2020 ilikuwa sh 150,000, mwaka 2021 sh 150,000, mwaka 2022 sh 30,000, na mwaka 2023 sh 3,000.
Wakulima Gratian John (50), Beatrice Edward (74) na Edwin Kazaura (51), wamesema mwaka huu wamepata hasara kubwa kutokana na kuporomoka kwa bei toka sh 30,000 mwaka uliopita hadi sh 3000 mwaka huu.
Mkulima wa kupigiwa mfano, Edwin Kazaura, amelima vanilla kila mahali ikiwemo kandokando ya nyumba na uwanja wa mbele ya nyumba huku akisanifu kwa ufundi wa mikono, uwekezaji anaosema umegharimu zaidi ya sh milioni
Gratian John amesema kutokana na anguko la bei, sasa ni vigumu kwaje kulihudumia shamba kama kuajiri vibarua wa kukata nyasi za kutandaza shambani, na kuchavusha maua, na kuwa ni ngumu sasa kulipa karo ya wanafunzi.
" Kilimo cha vanilla kinahitaji uwekezaji yaani mtaji, utaalam na soko.Tunamuomba waziri wa kilimo Hussein Bashe atuwezeshe mitaji ili tukaushe vanilla kitaalam na pia kununua mashine ya kukamua mafuta toka vanilla iliyokaushwa ili tuwauzie makampuni", amesema Edwin Kazaura.
Mwenekiti wa kijiji cha Ruhija Jasson Kamala, amesema kilimo cha vanilla kimekuwa kikihimizwa kwenye mikutano na ndio maana kumekuwa na hamasa kubwa ya kilimo hicho, na hivyo akaiomba serikali kufanya kila jitihada kuwatafutia masoko.
Aidha wakulima hao, wamemuomba waziri wa kilimo kuliingiza zao hilo kwenye mazao ya kimkakati, na kumuomba awatembelee kujionea mwenyewe hali ulivyo.
Licha ya anguko la bei, wakulima hao hawajakata tamaa,kwani kuna kikundi cha watu 20 wamejiunga pamoja na kukausha vanilla tani 1.5 ambayo tayari wameihifadhi kwenye vifungashio wakisubiri wanunuzi
Aidha wakulima wa vanilla wanao ushirika wao (AMCOS), na hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kutumia mtaji na mikopo iwapo watawezeshwa na serikali.
Juhudi za kumtafuta waziri wa kilimo kuhusu maombi ya wakulima wa Ruzinga zinaendelea.
Hata hivyo waziri huyo alishatangaza mpango wa serikali kushirikiana na kampuni ya NEI huko Kilimanjaro, yenye kiwanda cha kuchakata vanilla, kufungua kiwanda sampuli hiyo hapa Kagera, katika Chuo cha Kilimo Maruku, na hivyo kuwaondolea wakulima hasara ya kuharibikiwa mavuno yao.
No comments:
Post a Comment