SABA WAHOJIWA UDANGANYIFU WA MTIHANI DARASA LA SABA-MWANZA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 22 September 2023

SABA WAHOJIWA UDANGANYIFU WA MTIHANI DARASA LA SABA-MWANZA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewahoji watu saba kwa tuhuma za kosa la udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba kwa kuwachukua wanafunzi wa sekondari na kuwafanyisha mitihani hiyo kwa niaba ya wanafunzi wa darasa la saba.


Tukio hilo lilitokea tarehe 13.09.2023 muda wa saa nane mchana huko katika shule ya msingi Igulumuki, kata ya Igulumuki, tarafa ya Sengerema wakati kamati ya mitihani ya wilaya ya Sengerema ilipotembelea shule hiyo kwa ajili ukaguzi na kubaini kufanyika kwa udanganyifu huo ambapo mkondo namba mbili na namba tatu kulikuwa kumeingizwa wanafunzi wa sekondari watatu na kufanya mitihani ya darasa la saba.


Watuhumiwa waliokamatwa na wanaendelea kuhojiwa ni 1.Maiko Sheusi, miaka 35, mwalimu wa shule ya Sekondari Sima ambaye ni msimamizi mkuu wa mtihani shule ya msingi Igulumuki 2.Musa mwashihava, miaka 38, mwalimu wa shule ya sekondari Kilabela ambaye ni msimamizi wa mtihani mkondo namba 2, 3 Bonasi Balozi, miaka 33, mwalimu wa shule ya sekondari Buzilasoga ambaye alikuwa msimamizi wa mtihani mkondo namba 3, 4 Azizi Mohamed, miaka 36 ,Mwalimu wa taaluma, shule ya msingi Igulumuki , 5 Shadrack Bwana, miaka 14, mwanafunzi wa shule ya sekondari Sima, 6 Revocatus Paulo, miaka 14, mwanafunzi wa shule ya sekondari Sima. 7. Pendo Bukoma, miaka 14, mwanafunzi wa shule ya sekondari Sima, mkazi wa Igulumuki.


Kufuatia tukio hilo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Igulumuki aitwaye Amlesian Mahingu Mfungo aliweza kukimbia mpaka sasa Jeshi la Polisi tunaendelea na jitihada za kumsaka ili aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.


Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya upelelezi kukamilika. Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza pamoja na kutoa elimu, pia limeendelea kuimarisha ulinzi maeneo yote na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahalifu.


Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linafanya uchunguzi kufuatia taarifa zilizotolewa kwenye kikao cha kusikiliza kero siku ya tarehe 18.09.2023 kwamba kampuni iitwayo Alliance Global in Motion ambayo imefungua ofisi yake katika jengo la Rock City Mall wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza inayojihusisha na vitendo vya utapeli dhidi ya vijana wakitanzania 150 kwa kuwatoza fedha kwa kigezo cha kufanya biashara ya tiba lishe kwa njia ya mtandao huku wakiendelea kuwashawishi vijana wengine kujiunga kwenye biashara hiyo inayodaiwa kuwa ni yautapeli.


Uchunguzi huo ulianza tarehe 19.09.2023 kufuatia taarifa hizo kutoka kwa wananchi kwa kuwahoji watu mbalimbali wakiwemo wanachama 46 kati yao mabinti wawili wa kampuni hiyo kutoka mikoa mbalimbali. Aidha, tumeendelea kufuatilia uhalali wa kampuni hiyo pamoja na shughuli inazozifanya kwa mujibu wa sheria na katika uchunguzi huo tutashirikiana kwa ukaribu zaidi na tasisi nyingine za Serikali.


Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza tunawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi kuhusiana na malalamiko yaliyotolewa.

Imetolewa na:

Wilbrod W. Mutafugwa – SACP

Kamanda wa Polisi

Mkoa wa Mwanza

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso