Chifu Wa Kabila la Wasafwa mkoani Mbeya Rocket Mwanshinga.
UONGOZI wa kimila wa Kabila la Wasafwa la Mkoani Mbeya umewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma ya chanjoya Polio itakapokuwa inatekelezwa kwa kuhakikisha wanawatoa watoto wao badala ya kuwaficha.
Uongozi huo umesema utakuwa bega kwa bega na serika katika kuhakikisha kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio inayotarajiwa kutekelezwa kwenye mikoa sita nchini na Mkoa wa Mbeya ukiwa miongoni kuanzia Septemba 21 hadi 24 mwaka huu.
Chifu Mkuu wa Kabila la wasafwa,Rocket Mwanshinga amesema viongozi wa kimila hawako tayari kuona mtu yeyote anakwamisha kampeni hiyo kwa kueneza uongo juu ya chanjo na kuahidi kuchukua hatua stahiki dhidi ya atakayebainika.
Chifu Mwanshinga aliyasema hayo aliposhiriki Kikao cha Uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Polio Wilaya ya Mbeya kilichofanyika jana na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.
Alisema wao kama viongozi wa kimila wanaipongeza serikali kwa kukumbuka kuwatibu wananchi na kuwakinga dhidi ya maradhi ya poliyo aliyosema ni hatari kutokana na watoto kupooza.
Alisema ni jambo la kushukuru kwakuwa serikali inaonyesha moyo wa kuwalinda wananchi juu ya matatizo yanayoweza kuwaathiri na ndiyo sababu viongozi wa mila wako tayari kutangaza kuhamasisha kampeni hiyo katika pande zote.
“Tuko tayari na tutahamasisha machifu wote kwamba kila mmoja atoe mtoto aliyeko ndani kuanzia miaka mitano mpaka nane wote wapate chanjo. Hii ndiyo usalama wetu katika nchi yetu. Tunataka watu wetu wawe salama ndani ya Tanzania yetu.” Alisisitiza Chifu Mwanshinga.
Chifu huyo alisema faida ya wanajamii ni kuchanja ni pamoja na watu kutolewa au kukingwa na maradhi yaliyopo hivyo hakuna sababu ya kuwasababishia watoto kupata ulemavu wa kupooza au vifo.
“Kuna watu wapo walio na akili mbaya wanaosema chanjo inaleta madhara..yale mambo potofu sisi machifu hatuyataki… chanjo hii haiui ila inaookoa… wasiende kinyume nah ii chanjo.” Aliongeza.
Kwa mujibu wa Afisa Chanjo wa jiji la Mbeya, Christopher Mathias Chanjo ya Polio ina umuhimu mkubwa kwa watoto walio na umri chini ya miaka nane hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanachanjwa wakati zoezi hilo litakapofanyika.
Mathias aliwasihi pia wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu watakaopita kutoa huduma ya chanjo kwenye maeneo yao hususani zitakapokuwa zinawekwa alama kwenye nyumba ambazo kaya zake zitakuwa zimefikiwa na kupata huduma kama ilivyofanyika katika awamu zilizopita.
Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa aliwataka wadau wote wilayani hapa kutoa ushirikiano wa kina ili kufanikisha kampeni hiyo inayolenga kuwaweka watoto kwenye usalama zaidi kiafya.
Baadhi ya wakazi jijini Mbeya walimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa kwa hamasa iliyokwisha fanyika katika awamu nne zilizotangulia za utoaji wa Chanjo ya Polio wanayo imani mwamko sasa ni mkubwa na wengi watajitokea kuhakikisha watoto wanapata chanjo.
Wakazi hao walipongeza hatua ya watoa huduma kutumia njia ya kupita nyumba kwa nyumba na pia mikusanyiko ya watu wakisema inawezesha kuwafikia watoto wengi zaidi wakiwemo walio na wazazi au walezi wasio na uelewa wa kutosha kwakuwa wanapata fursa ya kuelimishwa na majirani kuliko wataalamu pekee.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya jijini Dodoma, Septemba nane mwaka huu ilieleza kuwa kati ya watoto milioni 3.2 wanaotarajiwa kupata chanjo ya Polio kwenye mikoa sita hapa nchini, Mkoa wa Mbeya utakuwa na watoto 614,346.
Mikoa mingine ni Kagera watoto 729,387, Kigoma 884,477, Katavi 227,862, Songwe 402,643 na Rukwa 391883 huku jumla ya watoa huduma 5,291 waliopewa mafunzo wakitarajiwa kuifanya kazi hiyo kwenye mikoa hiyo.
No comments:
Post a Comment