KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU AFAGILIA UWEKEZAJI WA SHABOUT NZEGA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 21 September 2023

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU AFAGILIA UWEKEZAJI WA SHABOUT NZEGA


Na Mwandishi wetu, Nzega


KIONGOZI wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim ameipongeza kampuni ya ASHARIQ CONSTRUCTION COMPANY LIMITED kwa uwekezaji mkubwa wa mradi wa maduka 74 uliopo Mjini Nzega Mkoani Tabora.


Kaim ametoa pongezi hizo akizungumza September 20 wakati mwenge wa uhuru ukiweka jiwe la msingi kwenye mradi huo wa majengo ya maduka ya SHABOUT Mjini Nzega.


Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu amesema uwekezaji wa mradi huo ni mkubwa na utaendelea kuukuza mji wa Nzega, utachochea maendeleo ya eneo hilo na kutoa ajira kwa wakazi wake.


“Rais wa Serikali ya awamu ya sita Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo tumieni fursa hii kuwekeza, tunatambua jitihada za mwekezaji huyu na mbio za mwenge wa uhuru kwa heshima kubwa tunaridhia kuweka jiwe la msingi la jengo hili,” amesema Kaim.


Mkurugenzi wa kampuni ya ASHARIQ CONSERVATION COMPANY LIMITED Rashed Shabout Said amesema mradi huo wa maduka 74 ulianza kujengwa mwezi Februari 2023 na unatarajiwa kukamilika Machi 2024.


Rashed amesema hadi mradi huo utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi 800,000,000 na hadi sasa umefikia asilimia 70 ya gharama za ujenzi kwa shilingi 560,000,000.


“Fedha hizo zimetokana na ujasiriamali katika kodi za biashara za maduka ya SHABOUT SHOPPING CENTRE na ukandarasi katika kampuni ya ujenzi,” amesema.


Amesema faida ya ujenzi huo ni pamoja na kuunga mkono sera ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuzitaka sekta binafsi kuwekeza ili kuongeza ajira ambapo wanatarajia kuajiri watumishi zaidi ya sita, watakaotoa huduma mbalimbali katika jengo hilo ingawa kwa sasa wakati ujenzi ukiendelea wameajiri vijana zaidi ya 15 ikiwa ni pamoja na wataalamu 3.


Amesema faida nyingine ya uwekezaji huo ni pamoja na kuufanya mji wa Nzega uvutie sambamba na kulipa tozo na kodi mbalimbali Serikalini.


“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kuruhusu uwekezaji kupitia sekta binafsi na kutia chachu kwa wawekezaji kutafuta mitaji,” amesema.


Mkuu wa Wilaya ya Nzega Naitapwaki Lemeya Tukai amepongeza uwekezaji huo uliofanywa na kampuni ya ASHARIQ CONSERVATION COMPANY LIMITED kuwa utachochea maendeleo ya mji wa Nzega.


“Tunaomba ukague mradi huu na ikikupendeza tunaomba utuwekee jiwe la msingi, mwenge wa uhuru hoyeeee tunza mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa,” amesema DC Tukai.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso