Balozi wa Tanzania Nigeria: Tunafanya jitihada za kumuokoa mtanzania aliyetekwa nyara Nigeria
Mtanzania Melkiori Dominick Mahinini, mwanafunzi wa upadri ametekwa nyara nchini Nigeria tangu Agosti 3, huku watekaji nyara wakidai fidia ya $70,000.
Taarifa ya Dayosisi katoliki ya Minna ilisema kuwa kijana huyo alitekwa nyara pamoja na Padri Paul Sanogo kutoka Burkina Faso.
Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana aliithibitishia BBC tukio hilo na kusema wawili hao walishambuliwa na kutekwa nyara na watu wasiojulikana wakiwa kwenye sherehe za upadrisho.
‘’Tulipokea kwa masikitiko taarifa za kutekwa nyara kwa kijana huyu na padri kutoka Burkina Faso katika jimbo la Minna hapa Nigeria. Bado alikuwa katika mafunzo ya ukuhani na theolojia. Alikuwa akihudhuria sherehe ya upadri katika mtaa huo walipovamiwa na watu wasiojulikana kwa silaha nzito, na risasi kadhaa zilifyatuliwa. Imepita siku tano tangu kutekwa nyara’’
Dk.Bana aliambia BBC Pia, ubalozi unawasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Nigeria ili kuhakikisha wanamuokoa yeye na kasisi huyo kutoka Burkina Faso.
‘’Tumekuwa katika mawasiliano na wizara ya mambo ya nje ya Nigeria, na tumewataka kushirikiana na maafisa wa usalama ili waweze kuwaokoa watu hawa kwa usalama''
Baba yake Melkiori Dominick, Bw Dominick Mahinini, aliambia gazeti la The Citizen kwamba ameiomba Wizara ya Mambo ya Nje kushirikiana na Kanisa kuhakikisha mwanawe anarejea nyumbani salama.
“Sina la kufanya zaidi ya kumwomba Mungu ampe uhai. Naomba msaada wa serikali katika suala hili,”
Utekaji nyara kwa ajili ya fidia ni biashara yenye faida kubwa nchini Nigeria.
Tangu 2011, watekaji nyara wamekusanya angalau $18m, na zaidi ya nusu yake kati ya 2016 na 2020, kwa mujibu wa shirika la SBM lililoko Lagos.
Chanzo:BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment