Mashabiki wa klabu ya Simba katika kijiji cha Nyanhembe wakimpokea mgeni rasmi Khamis Mgeja kwenye sherehe ya tawi lao kijijini hapo.
Khamis Mgeja akiwa na wanachama wa Simba katika kijiji cha Kiinza baada ya kusimamishwa msafara wake ili kuchangia harambee ya Zahanati, Simba day
Khamis Mgeja akizungumza na mashabiki wa Simba katika kijiji cha Kiinza waliosimamisha msafara wake wakati akielekea Nyanhembe kwenye sherehe ya Simba day
MASHABIKI wa soka wa klabu ya Simba katika Vijiji vya Kiinza na Nyanhembe vilivyopo Kata ya Kilago halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga vimeadhimisha sherehe ya “Simba day” kwa aina yake.
Sherehe za “Simba Day” zilizohudhuriwa na mwenyekiti wa zamani wa chama cha soka mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) Khamis Mgeja ambaye pia ni mwanachama wa klabu ya Simba na mdau wa michezo nchini.
Katika Kijiji cha Kiinza mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba walisheherekea na kufanya harambee kusaidia ujenzi wa miundombinu ya Zahati ya Kilago ambapo msafara wa Khamis Mgeja ulizuiliwa ili kuwaunga mkono na kuwachangia na wote kwa pamoja kwenye harambee hiyo waliwezesha kupatikana shilingi laki moja na Elfu sita mia tano (106,500).
Mgeja pia akiwa tawi la Simba Nyanhembe ambapo alikuwa mgeni rasmi wanachama na mashabiki hao kwa Pamoja wamechangia kiasi cha shilingi Elfu sabini na tatu kwa ajili ya kutengeneza ofisi ya tawi lao la Simba pia katika changizo hilo la harambee waliungwa mkono na watani zao wa Yanga.
Pia Khamis Mgeja ameahidi kuwachangia shilingi laki moja (100,000) kwa timu ya Nyanhembe Star ya kushiriki mashindano makubwa ya kitaifa ya Ndondo Cup ya Clouds FM mashindano yanayotarajiwa kufanyika wilayani Kahama ili kuwapa fursa vijana wenye vipaji kuonekana na kuweza kuchukuliwa na timu mbalimbali zinazoshiriki ligi kuu, daraja la kwanza na daraja la pili.
Mgeja amesema sherehe za “Simba day” zimefana sana na kuhamasika vijijini na mjini nchi nzima ambapo mwitikio mkubwa umeonekana kwa vitendo kitu ambacho kinasaidia maendeleo kwenye jamii ya kuwaweka Pamoja hivyo ni suala la kujivunia na kuliunga mkono.
Amewashauri mashabiki wa timu za Simba na Yanga kuendeleza utamaduni wa utani wa jadi na sio kuzalisha na kukuza uadui kitu ambacho kitaurudisha mpira wa Tanzania katika ngazi ya chini na kushindwa kufanya vizuri kimataifa na kuitangaza Tanzania.
Aidha amewaomba vilabu na wadau wa michezo kuwekeza katika soka la wanawake na vijana ili kuweza kupata mafanikio makubwa na mazuri kama yalivyo mataifa ya Senegal, Africa Kusini, Tunisia mengine ambayo yamejikita katika vituo vya kuzalisha wachezaji wazuri.
Hata hivyo Khamis Mgeja amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono kwa vitendo sekta ya michezo mbalimbali nchini huku akiwaomba wadau wa michezo kuchangamkia fursa ya Mheshimiwa Rais ya utashi wake kwa kumuunga mkono ili kusukuma maendeleo ya michezo na kupata mafanikio.
Mgeja amewaomba wadau kuwekeza kwenye michezo kwa kushirikiana na vyama vya mpira wa miguu huku akimuomba mkuu wa Wilaya ya Kahama na mkuu wa mkoa wa Shinyanga kuitisha kikao cha wadau wa michezo ili kujadili namna ya kupatikana timu ya ligi kuu wakiwemo wafanyabiashara na makampuni sambamba na migodi ya madini iliyomo mkoani Shinyanga kwani Shinyanga kupata timu ya ligi kuu inawezekana kinachohitajika ni ushirikiano wa Pamoja wenye nia njema.
No comments:
Post a Comment