MBUNGE JIMBO LA NKENGE, FLORENT KYOMBO AWAPA MATUMAINI KITONGOJI LUSHENYE, WILAYANI MISSENYI: MITUMBWI YA KISASA NA SHULE SHIKIZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 12 August 2023

MBUNGE JIMBO LA NKENGE, FLORENT KYOMBO AWAPA MATUMAINI KITONGOJI LUSHENYE, WILAYANI MISSENYI: MITUMBWI YA KISASA NA SHULE SHIKIZI

Mpango kabambe wa taifa wa kuhakikisha wanafunzi walioko pembezoni hasusani maeneo yasiyofikika kwa urahisi, wa kuanzisha shule shikizi kuwezesha wanafunzi wa maeneo hayo hasa madarasa ya awali, umegonga hodi katika kitongoji cha Lushenye, kijiji Gabulanga, kata ya Kassambya wilayani Missenyi.

Na Mutayoba Arbogast, Huheso Digital, Bukoba



Mbunge wa Jimbo la Nkenge Florent Kyombo, akiongea na wananchi na wanafunzi katika kitongoji cha Lushenye


Kitongoji hicho kilicho kandokando ya mto Kagera, kiko umbali wa takribani km 18 kufika makao makuu ya kijiji Gabulanga, na njia haipitiki wakati wote wa mwaka kwani nyakati za mvua hujaa maji, hivyo wananchi hulazimika kuvuka mto kwa mtumbwi wa makasia kwenda kijijini na kata jirani ya Bugorora kufuata huduma muhimu zikiwemo za elimu, afya, manunuzi nk.


Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wa kitongoji hicho, wakiwemo wale wenye umri chini ya miaka nane walio katika madarasa ya awali hadi darasa la nne hulazimika kuvuka mto wenye hatari ya viboko, mamba, nyoka na kuchafuka kwa mto, huku ikielezwa na uongozi wa kitongoji kwamba kuna nyakati wanajivusha wenyewe, kwa madai kuwa mwenye zamu ya kuwavusha amechelewa, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.


Baada ya kilio cha muda mrefu kuhusu suala hilo,mbunge awa jimbo la Nkenge, Florent Kyombo, akifuatana na Afisaelimu msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Missenyi, Warento Warento na viongozi wengine wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ametembelea kitongoji hicho kwa kuvuka mto huo kwa mtumbwi kutokea kijiji cha Bugorora.


Akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara tarehe 9 Agosti 2023, mh Kyombo amesema anasikitishwa na hali hiyo, na kubainisha kuwa serikali ilishatenga fedha kujenga vyumba viwili vya madarasa, lakini bahati mbaya ilikuwa nyakati za mvua na kitongoji hicho kilijaa maji hivyo haikuwezekana na fedha ikaelekezwa mahali pengine.


Hivyo akaahidi kazi hiyo ya ujenzi kuanza hivi karibuni mradi kijiji kitenge eneo linalofikika kwa urahisi , huku Afisa elimu akisisitiza atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha ujenzi huo wa vyumba viwili unafanikiwa.


Katika risala ya kitongoji hicho iliyosomwa mbele ya mbunge, jumla ya watoto 134 wenye umri wa kwenda shule hawaendi shule kutokana na kutokuwepo miundombinu ya elimu, huku wanafunzi wanaovuka mto kwenda Bugorora shule ya msingi na shule ya sekondari Nkenge (iliyoko kata Bugorora) ni 150.


Katika kukabiliana na changamoto ya kuvuka mto kwa mtumbwi wa kienyeji ambao hutumia takribani dakika 45 kuvuka mto, mbunge huyo ameahidi mfuko wa jimbo kugharamia mitumbwi miwili ya injini, mmoja mwaka huu na mwingine mwaka kesho.


Wanafunzi Justus Justinian na Agnes Erasto wanasema huvuka mto huo kwa hofu kubwa kwani kuna nyakati mto unachafuka maji yakiingia mtumbwini na pia mitumbwi ni hatarishi kwani wakati mwingine inakuwa na matobo yanayoingiza maji.


Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Hamza Sadiki, amemshukuru mbunge kwa ziara hiyo yenye matumaini kwao kufaidi matunda ya maendeleo


"Sisi ni kama tumefungiwa mahali, kwenda Gabulanga ni shughuli kwelikweli, kuvuka mto kwa mitumbwi yetu hii, nalo si jambo jepesi, sasa kitongoji kinafunguliwa na watoto wetu kwa hatua za mwanzo watasoma hapa hapa, tunamshukuru sana mbunge wetu", alisema mwenyekiti huyo.


Hadi kufikia Desemba 2022, serikali ilitumia jumla ya shillingi bilioni 60 kujenga vyumba vya madarasa 3,000 ya shule shikizi nchini kote.


Mkakati wa shule shikizi unalenga kuwasaidia watoto wa pembezoni kujumuika na watoto wote Tanzania kuwa kwenye mwelekeo sahihi wa kuzifikia ndoto zao.


Mbunge Florent Kyombo (aliyevaa miwani meusi) pamoja na timu yake walipokuwa wakivuka mto Kagera kwenda kitongoji cha Lushenye


Mwandishi wa habari hii (mwenye koti jeusi), wakati fulani mwaka 2018 alivuka mto huo kwenda kigongoji Lushenye kufuatila mustakabali wa elimu kwa watoto wa kitongoji hicho na huduma nyingine za kijamii

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso