WAKATI SERIKALI IKITANGAZA RASMI KUTOKOMEZWA UGONJWA WA MARBURG MKOANI KAGERA, WIZARA YA AFYA YAELEZA KUGUSWA NA KIFO CHA MTOTO MDOGO, HUKU WATATU WALIOKUWA WAMELAZWA WAKIPONA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 3 June 2023

WAKATI SERIKALI IKITANGAZA RASMI KUTOKOMEZWA UGONJWA WA MARBURG MKOANI KAGERA, WIZARA YA AFYA YAELEZA KUGUSWA NA KIFO CHA MTOTO MDOGO, HUKU WATATU WALIOKUWA WAMELAZWA WAKIPONA


Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameagiza wataalam wa wizara hiyo kuendelea kuchunguza na kufanya tathmini nini hasa kilisababisha kifo cha mtoto wa miezi 18 kufariki kutokana na ugonjwa wa Marburg uliotokea katika kata za Maruku na Kanyangereko,wilaya ya Bukoba mkoani Kagera mwezi Machi 2023, licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na serikali pamoja na Wizara ya Afya, kuokoa maisha yake.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akitangaza rasmi kutokomezwa kwa ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera Kushoto mwenye miwani ni Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, na Kulia ni Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera, Toba Nguvila


Na Mutayoba Arbogast, Huheso digita Bukoba


Waziri Ummy ameyasema hayo Juni 02,mwaka huu mjini Bukoba katika maadhimisho ya kutangazia rasmi nchi na jumuiya za kimataifa, kumalizika kwa ugonjwa wa mlipuko mkoani Kagera, uliosababisha vifo vya watu sita.


"Watu waliothibitika kufariki kwa ugonjwa huo ni sita, lakini vifo vitano vilitokea nje ya hospitali. Jumla ya watu waliothibitika kuwa na ugonjwa huu walikuwa tisa. Sasa wale tuliowaweka karantini watatu walipona, akiwemo daktari wetu Mahona Madulu. Bahati mbaya tulimpoteza mtu mmoja ambaye ni huyo mtoto mdogo.Inasikitisha", alisema Ummy Mwalimu akimgeukia kwa simanzi mwakilishi wa Shirika la watoto ulimwenguni hapa Tanzania (UNICEF), Shalini Bahuguna.


Amewataka wataalam kuendelea kuchunguza sababu ya kifo cha mtoto huyo licha ya kuwepo huduma nzuri za kitaalam na kibingwa zilizoweza kuwaokoa wagonjwa wengine watatu ili matokeo yatumike kama somo endapo utatokea mlipuko mwingine.


"Ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi, Serikali, watumishi wa idara ya Afya na wadau kutoka ndani na nje ya nchi ndio umechangia kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huu na kwa sasa tunasherehekea hivyo, natangaza leo ugonjwa huu umeisha, Tanzania ni salama ila tusibweteke tuendelee kujikinga na kutoa taarifa pale tunapoona mambo tusiyoyaelewa", anasema Waziri Ummy


Amesema mlipuko huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza katika kata za Maruku na Kanyangereko Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Machi 19 mwaka huu kama ugonjwa usiojulikana kabla ya kuthibitishwa ulikuwa ni Marburg ambapo walipatikana wagonjwa tisa watatu wamepona na sita walipoteza maisha.


Amesema miongoni vifo hivyo ni vya watu wanne kutoka familia moja na pia mtumishi mmoja wa Afya ambaye alikuwa mtaalam wa maabara katika kituo cha Afya Maruku aliyehudumia wagonjwa wa kwanza, (ambao hawakulazwa) na huyo mtoto mdogo wa miezi 18 aliyefia hospitali na hivyo akasema wanaendelea kufanya uchunguzi kama Serikali ili wajue kiini cha mlipuko huo.


Mganga mkuu wa Serikali Prof.Tumaini Nagu amesema mafanikio hayo yametokana na kuwa walipata taarifa mapema na kuchukua hatua mapema pia amewashukuru wadau mbalimbali walioshirikiana na Serikali katika mapambano hayo ikiwemo shirika la Afya duniani (WHO), UNICEF, US CDC na Africa CDC.


Kwa upande wake mhanga wa ugonjwa wa Marburg ambaye alipona, alikuwa mtaalamu wa afya kituo afya Maruku Dk Mahona Madulu ametoa shukrani kwa madaktari wote waliosaidia kupona kwake na akawatahadharisha wataalamu wenzake wanapokuwa wanatimiza majukumu yao kuchukua tahadhali.


Dr Zabulon Yoti, mwakilishi wa Shirika la Afya hapa nchini (WHO), Shalini Bahuguna, mwakilishi wa Shirika la watoto ulimwenguni(UNICEF) na Dr Ahmed Ogwell Ouma, Naibu mkurugenzi mkuu wa Africa CDC, wakitoa salaam zao kwa nyakati tofauti wameishukuru serikali, wizara ya Afya na wananchi kwa jitihada walizofanya, na pia kuwashirikisha na kufanya kazi sambamba kuokoa maisha na kuudhibiti ugonjwa huo unaoenea kwa kasi.


Serikali imetenga Sh bilioni mbili kwa kuanzia ili kujenga kituo kikubwa cha kuhudumia wahonjwa wa magonjwa ya mlipuko mkoani Kagera na pia kuboresha huduma mbalimbali za afya zikiwamo za mama na mtoto.

Kutoka Kushoto ni Dr Ahmed Ogwell Ouma , Naibu mkurugenzi mkuu wa Afrika CDC, na Shalini Bahuguna, mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso