VIONGOZI NA WANANCHI WAHIMIZWA KUWA NA JITIHADA ZA PAMOJA KATIKA KUKABILIANA NA VIFO VYA AKINA MAMA NA WATOTO, WAKATI WA KUJIFUNGUA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 17 June 2023

VIONGOZI NA WANANCHI WAHIMIZWA KUWA NA JITIHADA ZA PAMOJA KATIKA KUKABILIANA NA VIFO VYA AKINA MAMA NA WATOTO, WAKATI WA KUJIFUNGUA

Viongozi na wananchi mkoani Kagera wamehimizwa kuendeleza jitihada za pamoja katika kukabiliana na vifo vya akina mama wajawazito wanapojifungua kutokana na sababu mbalimbali, ambazo pia huwaathiri watoto na kusababisha vifo wakiwa tumboni au baada ya kuzaliwa.


 Na Mutayoba Arbogast, HUHESO DIGITAL BLOG, Bukoba


Mratibu msimamizi wa mfumo wa m-mama kitaifa Dr Naibu Nkongwa


Mratibu msimamizi wa mfumo wa 'M-Mama' kitaifa, Dr Naibu Nkongwa  amehimiza juu ya ushirikiano huo wakati wa kikao kazi cha kuutambulisha mfumo huo mkoani Kagera ambacho kimefanyika ukumbi wa ELCT Hotel, manispaa ya Bukoba wiki hii, kikiwashirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi ofisi ya mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za wilaya, maafisa maendeleo ya jamii na wataalam wa afya, viongozi wa dini, wazee maarufu na wengineo.


"Vifo vya akina mama wajawazito na watoto vipo na tunaviona.Sisi viongozi ndiyo chachu ya kukabiliana na vifo hivi. Jitihada za pamoja zinahitajika", amesema Dr Nkongwa.


Mfumo huo wa m-mama unaotumia teknolojia ya kisasa uliobuniwa na kampuni ya Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, unalenga kutatua changamoto ya usafiri wa dharura kwa akina mama wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga kupitia huduma hiyo iliyounganishwa kwa watoa huduma za afya kwa pamoja.


Mratibu wa  mpango wa mama na mtoto mkoa wa Kagera, Neema Kyamba, akiongea  katika kikao hicho amesema akina mama wajawazito 42 katika kipindi cha mwaka 2022 walipoteza maisha.

Mratibu wa mpango wa mama na mtoto mkoani Kagera, Neema Kyamba

"Visababishi vikuu vya vifo vya mama wajawazito ni kutokwa damu nyingi wakati na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, mimba kuharibika, na matatizo mengine. Kwa upande wa watoto wachanga ni kushindwa kupumua, kuzaliwa na uzito pungufu, uambukizo wa mama nk", amesema Kyamba.


Amesema mkoa wa Kagera unavyo vituo 27 vinavyoweza kutoa upasuaji wa dharura  ambapo mwaka 2022 akina mama 2,500 kati ya zaidi ya 9,000 walifanyiwa upasuaji wa dharura.


Mkoa unayo magari ya dharura (Ambulances) 28 ambayo yalisafirisha akina mama wajawazito na watoto 1300 kwa mwaka 2022 kutoka zahanati na vituo vya afya kwenda hospitali walizoandikiwa rufaa, huku mahitaji mkoa ukiwa na mahitaji ya magari zaidi ya 55.


Mratibu huyo wa mpango wa mama na mtoto mkoani Kagera, ameendelea kusema kuwa vifo vya watoto wachanga vimeendelea kuongezeka ambapo kwa mwaka 2022 kulikuwa na vifo 185 kutoka vifo158 mwaka 2021.


"Hapa kuna sehemu kubwa ya kuifanyia kazi maana vifo hivi vya watoto wachanga vinaongezeka, na inaonekana baadhi ya watoto hao wakati mama zao wakiwa wako kwenye uchungu walikuwa hai. Hii inatuonesha kuwa akina mama wangesafirishwa kwa haraka kuwawezesha kupata huduma, watoto hao wasingepoteza maisha.", amesema Kyamba, akiongeza kuwa kwa kipindi cha Januari - Aprili 2023 kulikuwa na vifo vya watoto wachanga13, ambapo   si mwendelezo mzuri.


Amesema vituo vya kutoa huduma  vya serikali vimekuwa vikiongezeka hadi kufikia 366 na ushirikiano uliopo kwa vituo vya binafsi ni fursa kubwa kwa mkoa, na kuwa uanzishwaji wa mfumo wa m-mama utaongeza fursa nyingi katika kupata takwimu nzuri za rufaa na kujua nini kinaendelea zaidi ya ilivyo sasa.


"Changamoto bado ni  kuwa vifo bado ni vingi, baadhi ya miundo mbinu ni hafifu, na  magari bado ni machache huku mengine yakiwa chakavu, hivyo tushirikiane katika kukabiliana na changamoto hizi", amesema Kyamba.


Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera, Toba Nguvila, amesema ukosefu wa uhakika wa usafiri wa dharura kutoka kwenye jamii kwenda vituo vya kutolea huduma ni moja ya sababu za vifo hivyo na kuwa mkoa unaendelea  kushirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo.


Tafiti zinaonesha kuwa kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa mwaka 2022 kimefika vifo 43 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai ukilinganisha na vifo 67 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai ilivyokuwa kwenye Utafiti uliofanyika mwaka 2015/2016.


Hayo yalisemwa Februari 7, 2023 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa matokea muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa Mwaka 2022 uliofanyika katika ofisi za Taifa ya Takwimu Jijini Dodoma.


Programu Jumuishi ya Taifa inayoangazia malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) likiwemo suala la uzazi salama, imelinukuu Shirika la Kikatoliki linalotoa misaada ya kibinadamu la Catholic Relief Service (CRS),  linasema msongo wa mawazo kwa baadhi ya akina mama wajawazito na baada ya kujifungua  huwaathiri kiasi cha kusababisha vifo na athari nyingine za kimakuzi kwa watoto chini miaka nane.Katika utafiti uliofanywa na shirika hilo  katika wilaya za Geita, Sengerema na Buchosa asilimia 18 ya akina mama wenye watoto wachanga waliofikiwa,walikuwa na msongo wa mawazo, ambao walihitaji msaada wa jamii kurudia hali zao.

Baadhi ya washiriki(wakuu wa wilaya) wakati wa kikao kuutambulisha mfumo wa m-mama

 Afisa Tawala wa mkoa wa Kagera,Toba Nguvila


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso