Idadi ya wanaume wanaokabiliwa na matatizo ya kushindwa kutungisha mimba inaongezeka nchini, huku ikitajwa kuwa wagumu kukubali vipimo, wakihofia aina ya upimaji na wenye mapokeo hasi ya majibu yao ikilinganishwa na wanawake.
Kwa mujibu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), robo tatu ya matatizo ya ugumba kati ya wanawake zaidi ya 1,200 wanaofika kila mwaka kuhitaji usaidizi wa upandikizaji mimba yanawahusu wanaume.
Wengi mbegu zao huwa hafifu, zisizo na mwendo na nguvu ya kuhimili kulifikia yai kwa ajili ya utungishaji mimba, hali inayochangiwa na ulaji usiofaa, aina ya kazi wanazofanya, magonjwa ya zinaa katika via vya uzazi na mabadiliko ya homoni.
Hayo yamebainika wakati Muhimbili ikiwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza upandikizaji mimba kupitia maabara Novemba mwaka huu, baada ya mchakato muhimu kukamilika.
“Wanaume kwa sasa wana matatizo mengi na magumu kuliko wanawake na kwa kuwa jamii inaamini mwanamke ndiye anayezaa, wanaokuja hospitali ni wanawake na tunaendelea kuwasihi wawalete wanaume, hasa pale unapompima na unamkuta hana shida yoyote.
“Kuna wengine anakwambia hawezi kuja kwa daktari, kwa hiyo unaamua kuanza naye,” alisema Dk Ngarima.
Alisema wanaume wakifika hospitali mara nyingi hukosa ushirikiano, ijapokuwa wachache wanakubali maelekezo na wanasikiliza na kwamba wapo ambao hawafiki kabisa na wanaokwenda wana haraka ya kuondoka.
“Wengi kipimo cha kutoa mbegu hawakipendi, wanaona kama kinawaaibisha, kwamba atoe mbegu akiwa hayupo na mwanamke wanaona ni kigumu na kinawashushia hadhi yao, lakini sisi tupo katika matibabu kwa kuwa kutoa mbegu ni tendo la siku moja, maana inabidi zitolewe kwa kujichua,” alisema.
Dk Ngarina alisema majibu yanapotoka wanawake wapo tayari kuyapokea, lakini ni changamoto kubwa kwa wanaume, wengi wanayakataa na wengine wanapata msongo wa mawazo.
“Hawapo tayari, ukimwambia ana shida huenda ikamfanya asiweze kupata mtoto ni habari mbaya sana kwao, wengi wanaipokea vibaya, wanapata huzuni, msongo wa mawazo, wanafanya maamuzi magumu,” alisema.
Alisisitiza kuwa sayansi ipo na namna ya kusaidia ipo, ni kiasi cha kutulia na huwa wanawashauri nini cha kufanya kwa kuwa hata kama mwanaume ana mbegu moja inaweza kuchukuliwa akapandikizwa mke.
No comments:
Post a Comment