Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa makatibu tawala wa wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kwa kuteua wapya, kuwahamisha vituo na wengine kuachwa katika vituo vyao vya awali.
“Katika mabadiliko hayo, Rais amefanya uteuzi mpya pamoja na kuwahamisha vituo vya kazi baadhi ya makatibu tawala na wakurugenzi watendaji,” inaeleza taarifa hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Baadhi ya wateule wapya katika nafasi ya katibu tawala wa wilaya ni pamoja na Theresia Mtewele anayekwenda Wilaya ya Kasulu. Mtewele ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.
Wengine walioteuliwa kutoka CCM Makao Makuu, Said Nguya ambaye anakwenda Wilaya ya Mvomero pamoja na Ruth Magufuli ambaye anakuwa katibu tawala wa Wilaya ya Morogoro.
Kwa upande wa wakurugenzi, Geofrey Nnauye ameteuliwa kuwa mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Newala na Nuru Kindamba akiteuliwa kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Baadhi ya wakurugenzi walioachwa katika vituo vyao vya kazi ni pamoja na Spora Liana anayebaki katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na Saitoti Zelothe ambaye anabaki kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Aron Kagurumjuli aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, ameteuliwa tena kuwa mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Mwanza.
Habari zaidi:
No comments:
Post a Comment