IMEBAINIKA kuwa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imekumbwa na mmomonyoko wa maadili kwa watoto kukosa heshima pamoja na kujitambua katika kutatua changamoto zao zinazowakumba katika jamii.
Hayo yamesemwa katika kikao cha utoaji taarifa ya utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Development Aids Prevention Association (TADEPA) 25/05/2023 kupitia mradi wa Alive ambao ulijikita kufanya utafiti kwa watoto wa miaka 13-17 ukishirikisha wadau mbalimbali pamoja na serikali.
Meneja kutoka TADEPA, Penina Petro amesema mradi huo ulikuwa unafanya kazi katika Kata kumi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na Ushetu Kata moja ambao ulikuwa ukiangazia stadi za maisha kwa watoto kati ya umri wa miaka 13-17 na uwezo wao wa kutatua changamoto zinazowakabili.
Penina amesema utafiti walioufanya kuanzia Julai hadi Oktoba 2022 wamebaini kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa kundi hilo sambamba na uwezo mdogo wa kujitambua ikiwemo kutatua changamoto (matatizo) yao kwani limekuwa likificha taarifa za ukatili dhidi yao.
Penina ameongeza kuwa utafiti wao walikuwa wakiangalia pia heshima kwa watoto na matumizi ya mitandao ambapo wamebaini kuna tatizo kubwa la ‘heshima’ baada ya watoto wengi kukiri hivyo amewashauri wazazi na walezi kujikita katika malezi ya watoto na sio makuzi jambo ambalo litasaidia kujenga jamii bora.
“Kila mmoja wetu kwenye kikao chetu ameona ni namna gani ya kuwalea watoto na sio tu kuwaachia wazazi, viongozi wa serikali, Siasa, viongozi wa dini au walimu hivyo kila mmoja kuanzia ngazi ya kaya ushirikiano wa malezi kuhakikisha unaboreshwa”.
Mwakilishi wa shirika la Milele Zanzibar Foundation ambao ni waratibu wa mradi wa Alive, Hasna Kingu amesema katika upimaji wa stadi za maisha kwa watoto ulifanyika kwa zaidi ya halmashauri 34 kwa Tanzania bara ambapo wamegundua tuko nyuma katika maadili hivyo jamii inapaswa kusimama imara katika malezi.
Amesema wamewakutanisha wadau mbalimbali ili kujua nini kifanyike katika malezi ya watoto ambapo watoto wengi wanajiingiza katika vitendo viovu na wanakaa kimya na wazazi wengi hawafahamu ni maana ya stadi za maisha hivyo tunawawezesha namna ya kumtambua mtoto alien a changamoto.
Baadhi ya wazazi na walezi wakiwemo waliohudhuria kikao hicho akiwemo Aivela Audax na Jamila Kajehe wameshauri kuwa katika malezi ya watoto wazazi wengi wamejikita katika shughuli zao na kushindwa kuwa karibu na watoto kitu ambacho kinapelekea mmomomonyko wa maadili.
Wamewashauri wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya watoto wawapo nyumbani au shuleni kwani muda mwingi wazazi wamekuwa wakiamini walimu ndio jukumu lao la kufundisha maadili jambo ambalo sio sawa kwani kila upande unapaswa kucheza eneo lake huku wakiomba kuanzishwa kwa mitaala ya elimu za stadi za maisha shuleni.
Aidha mwakilishi wa katibu tawala wa Wilaya ya Kahama, Vicent Ndesekio ameishauri jamii kuamini kuwa maadili bora yanajengwa kuanzia nyumbani hivyo kila mtu ana wajibu wa kusimamia maadili huku akiziomba mamlaka zingine za serikali zikiwemo za kisheria kuendelea kusimamia sheria zinazopingana na maadili ya kitanzania ili wanaobainika wachukuliwe hatua.
No comments:
Post a Comment