Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesaini Mkataba wa kuzalisha umeme wa JUA kwa kutumia Teknolojia ya SOLAR PHOTO VOLTAIC wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 ambapo itatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza megawati 50 na kisha megawati 100 utajengwa katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga mradi unaotajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea hapa nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba pamoja na Mkuu wa Mkoa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme wakishuhudia utiaji saini kwenye mradi wa Uzalishaji umeme mkoani Shinyanga
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba alisema kuwa kusainiwa kwa mradi huu ni sehemu ya mipango ya mapinduzi katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mseto katika Sekta ya Nishati nchini ili kuweza kufikia lengo la kuwa na megawati 5000 kwenye Gridi ya Taifa ifikapo 2025.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ambaye ndiye mwenyeji wa mradi huo katika Mkoa huo alimshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Munngano wa Tanzania, Wizara ya Nishati na Tanesco kwa kuwezesha utiaji saini wa mradi huo muhimu zaidi ambao utakwenda kuinufaisha Shinyanga kwa kuzalisha nishati, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa wananchi kwa ujumla.
"Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kabisa kipekee kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Nishati na Tanesco kwa kuwesesha utiaji saini wa mkataba huu leo, hii ni furaha sana kwetu kwakuwa pamoja na kuzalisha umeme lakini pia mradi unakwenda kuongeza ajira na kuinua uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na pato la Taifa kwa ujumla," alisema Mhe. Mndeme.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme wakati wa kutia saini katika uzinduzi wa mradi wa uzalishaji umeme jua
Hafla ya utiaji saini wa mkataba wa kuzalisha umeme kwa teknolojia ya SOLAR PHOTO VOLTAIC imeongozwa na Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mhe. Christina Mndeme ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kaimu Mwenyekiti Kamati ya Nishati na Madini ya Kudumu ya Bunge Mhe. Judith Kapinga, Mhe. Boniphace Butondo Mbunge Jimbo la Kishapu na wadau mbalimbali.
No comments:
Post a Comment