WITO WATOLEWA KUWADADISI NA KUWASIKILIZA WATOTO KATIKA KULINDA USALAMA WAO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 13 April 2023

WITO WATOLEWA KUWADADISI NA KUWASIKILIZA WATOTO KATIKA KULINDA USALAMA WAO


WAZAZI, walezi na jamii kwa jumla wametakiwa kuwa makini katika kuwadadisi na kuwasikiliza watoto wao ili kujua matatizo na matarajio yao na hatimaye waweze kubaini mambo muhimu ya kuwatimizia katika kulinda usalama wao.

Picha ya pamoja ya waliohudhuria kongamano la kuadhimisha Siku ya watoto wa mitaani ulimwenguni,lililoandaliwa na shirika la Hekima.Kutoka kulia ni Mkugenzi mtendaji wa Hekima, Chui Majaliwa, Afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Bukoba,Hellen Rocky na Afisa dawati la jinsia wilaya ya Bukoba,Sgt Dorothea Samwel.



Na Mutayoba Arbogast,HUHESO DIGITAL,Bukoba


Wito huo umetolewa na Afisa wa Jeshi la Polisi, Dawati la Jinsia wa wilaya ya Bukoba, Sajenti Dorothea Samwel wakati akiwasilisha Uzoefu wa Dawati la Jinsia juu ya kesi za watoto wa mtaani,katika maadhimisho ya Siku ya Watoto wa mtaani Ulimwenguni,yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali liitwalo Hekima lililoko manispaa ya Bukoba, lililowakutanisha mashirika rafiki yanayohusika na masuala ya watoto, wadau wa elimu, maafisa wa Jeshi la Polisi na Uhamiaji, na baadhi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, maarufu kama 'Watoto wa mtaani'.


Sajenti Dorothea amesema si kweli kwamba watoto wote wa mtaani wanatoka kwenye familia zenye mazingira magumu ya umaskini,bali wengine wanatoka katika familia zenye uwezo mzuri kimapato, ila kutokana na kutosikilizwa wanapoeleza matatizo yao,au wazazi na walezi kutowadadisi na kuwafuatilia kujua masahibu yao,hutoroka kwenda mijini.


Alitolea mfano wa mtoto wa kiume aliyekuwa akisoma shule nzuri ya binafsi yenye gharama kubwa, akawaeleza wazazi ahamishwe kutoka shule hiyo,lakini wazazi walipuuza hadi mtoto akatoroka shule na kuja mtaani na alipodadisiwa kirafiki alieleza kuwa alikuwa 'akiingiliwa' na wanafunzi wenzake.


Kuhusu watoto wanaobainika kujihusisha na masuala ya kijinai, Jeshi la polisi linawajenga kisaikolojia,kuwapa stadi za maisha na kuwashughulisha, na hatimaye wanabadilika kuwa raia wema.


Mwenyekiti wa mtaa wa Buyekera, manispaa ya Bukoba, Hellena Baligamba, amelishukuru shirika la Hekima kwa kukubali kumpokea mtoto wa miaka nane(jina la mtoto linahifadhiwa),ambaye alitelekezwa na mama yake,na shirika lilimhudumia kila kitu kwa mahitaji ya shule.


Mkurugenzi wa shirika la Hekima, Chui Majaliwa amesema shirika lake linawahudumia watoto 25 ambao wanafunzwa stadi mbalimbali,lakini lengo lao kubwa ni kuwabaini watoto wanaoishi mtaani na kuwaunganisha na familia zao.


Hadi kufikia mwezi Machi 2023 shirika limefanikiwa kuwaunganisha watoto 35 na familia zao, huku watoto nane wakirejea shuleni.


Amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na watoto 437,500 wanaoishi mtaani.


Ameiomba serikali na wafadhili kulisaidia shirika lake kujenga kituo cha kuwahifadhi watoto hao kabla ya kuunganishwa na familia zao kwani kwa sasa watoto hao,baada ya kufundishwa stadi za kazi na kupata mlo wa mchana,usiku hurejea mitaani kwa kuwa hakuna mahali pa kulala kituoni.


Mmoja wa watoto hao(jina linahifadhiwa), amewaambia washiriki kuwa miongoni mwa matatizo wanayopata ni kukosa chakula, kupigwa na hata 'kufanyiwa kitu mbaya' na watoto waliowazidi umri na hata watu wazima.


Mshiriki, Dk Imani Tinda, ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Tanzania youth with new hope in life organisation (TAYONEHO), amesema upo uhitaji mkubwa wa kujenga kituo cha kusuluhisha migogoro (Conflict Resolution Centre) mkoani Kagera ili kupunguza migogoro ya wazazi inayowakimbiza watoto majumbani.


Mgeni rasmi, Hellen Rocky ambaye ni Afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Bukoba, aliyemwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa manispaa, amewahimiza wazazi na walezi wote kushirikiana na serikali katika makuzi na malezi bora ya watoto yatakayowaepusha na vitendo viovu, na kuwa serikali imeendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika ulinzi na usalama wa mtoto ili kutokomeza ukatili dhidi yao.


Amesema serikali inaridhishwa na utendaji kazi wa mashirika wilayani humo, pia akayataka mashirika yaendelee kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.


Takwimu zilizotolewa na Shirika la kuhudumia watoto ulimwenguni (UNICEF) mwaka 1989, kulikuwa na watoto milioni 100 wa mitaani duniani kote.


Watoto hao ambao miongoni mwao wako chini ya miaka nane,umri ambao ni muhimu katika maendeleo ya awali ya mtoto, hukosa haki mbalimbali zikiwemo za kupata elimu na kutofanyiwa ukatili.

Mmoja wa wafadhili wa Hekima,akiteta na watoto waliohudhuria kongamano.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso