WAZAZI NA WALEZI WASHAURIWA KUPUNGUZA 'MIJUBULO' NA 'KULA BATA',BADALA YAKE WAWEKEZE KUCHANGIA CHAKULA SHULENI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 7 February 2023

WAZAZI NA WALEZI WASHAURIWA KUPUNGUZA 'MIJUBULO' NA 'KULA BATA',BADALA YAKE WAWEKEZE KUCHANGIA CHAKULA SHULENI


WAZAZI na walezi katika kata ya Bakoba,manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameshauriwa kupunguza kuhudhuria 'mijubulo'(kitchen party-shughuli za kufundwa mwali au sherehe ya kapu) kwa wanawake,na wanaume kupunguza 'kula bata' kwa maana ya kutumia fedha kufanya starehe,badala yake wachangie mpango wa chakula shuleni,ili wanafunzi wafuatilie masomo yao kwa ukamilifu.


Diwani wa kata ya Bakoba,manispaa ya Bukoba,Shabani Rashid akiwa katika kikao cha wazazi,walezi na wadau wa elimu kujadili juu ya uchangiaji chakula shuleni

Na Mutayoba Arbogast,HUHESO DIGITAL BLOG,Bukoba


Wito huo umetolewa hivi karibuni na diwani wa kata ya Bakoba,Shabani Rashid,wakati akizungumza na wazazi,walezi na wadau wa elimu wa shule za msingi za Bunena na Buyekera,na shule ya sekondari Bakoba.


"Ndiyo,tunasema hali ya uchumi ni ngumu,hali hii haiko Tanzania tu,ipo kila mahali na hii ni kutokana na vita ya Urusi na Ukraine. Hali hii isitufanye tubweteke kutowachangia wanafunzi kupata chakula shuleni,tulichukue kwamba ni jukumu mahsusi kama tunavyohangaikia mambo mengine ya kuinua familia zetu",amesema diwani huyo.


Alisema lazima kupunguza matumizi ili kuendana na hali halisi.


"Akina mama kama ulikuwa unahudhuria mijubulo sita punguza ubaki na mitatu,akina baba punguza kula bata,tuwekeze kwenye watoto wetu",amesema diwani Rashid.


Wazazi hao kwa pamoja wamekubaliana kuchangia sh 12,000 kwa mwezi kwa ajili ya ugali na maharage kwa wanafunzi


Hassan Byeyombo,ambaye ni mjumbe wa bodi ya shule ya msingi Buyekera na mzazi wa wanafunzi wawili shuleni hapo,amesema wameondokana na suala la wanafunzi kupata uji shuleni na sasa wamekwenda na agizo la serikali la kupata chakula shuleni.


kwamba shule yake wanafunzi walikuwa wanapata uji,lakini wazazi wengine walikuwa wanasuasua kuchangia,maana zaidi ya wanafunzi 1320 shuleni hapo ni kama wanafunzi 200 hivi waliokuwa wanakunywa uji.


"Sasa wazazi wamekubali kubadilika,wameahidi na watatekeleza",amesema mjumbe huyo wa bodi.


Alipoulizwa juu ya hali ya wanafuzi wa madarsa ya awali watapataje hicho chakula ambacho kwa kawaida kitakuwa tayari saa za mchana ilhali wao huruhusiwa kutoka shuleni saa tano,ambapo chakula hakitakuwa tayari,Afisaelimu wa kata ya Bakoba,Aneth Mashulano,amesema lengo ni watoto wote kupata chakula shuleni.


Amesema kuwa madarasa ya awali,la kwanza na la pili hutoka shule saa za asubuhi,lakini kwa mpango huu,itabidi walimu wavute muda na kuendelea nao hadi saa sita adhuhuri ili wote wapate chakula.


"Unajua hata wanafunzi hawa wa madarasa ya chini,hata wanapoondoka muda wao wa kawaida,wakati mwingine kule nyumbani wazazi na walezi wapo mitaani kuchakarika na ujasiriamali,wala hata watoto hawakuti chakula nyumbani,wengine wanapita tu mitaani kuchezacheza",amesema Afisaelimu huyo wa kata.


Kwa mujibu wa Waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 na Mwongozo wa Kitaifa wa huduma ya chakula na lishe shuleni, wa mwaka 2021,vinazungumzia umuhimu kuwa utoaji wa chakula na lishe shuleni kuna uhusiano kati ya afya ya mwanafunzi na maendeleo ya kitaaluma.

wazazi,walezi na wadau wa elimu katika kata Bakoba wakijadili juu ya elimu na upatikanaji wa chakula shuleni katika kuimarisha afya na maendeleo kitaaluma.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso