MWANAFUNZI wa darasa la awali (jina lake linahifadhiwa) anayeelezwa alikuwa mwanafunzi wa darasa la awali mwaka huu 2023,katika shule ya msingi Kashai,manispaa ya Bukoba,ambaye amekuwa akikataa kwenda shule kwa kuwa wazazi wameshindwa kuchangia mpango wa chakula shuleni,amepata msaada wa kuhamishiwa shule ya bweni ya Mushemba Trinity school,iliyoko wilaya ya Bukoba, itakayomgharamia mahitaji yote ya shule.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali Mushemba Trinity school
Na Mutayoba Arbogast,HUHESO DIGITAL,Bukoba
Mkurugenzi wa shule hiyo ya msingi inayopokea wanafunzi wa bweni na kutwa,Lena Mushemba ,amesema wameamua kumsaidia mtoto huyo baada ya kuguswa na hali ya mtoto huyo,iliyoonesha anapenda shule sana,lakini wazazi hawakuwa na uwezo wa kuchangia chakula shuleni,hivyo alikuwa mpweke wakati wenzake wanapata chochote yeye ameangalia tu.
"Tulipata taarifa kutoka kwa wanajamii kuwa kuna mtoto mdogo anazurura mitaani na kuwa ni mwanafunzi wa darasa la awali anayetoka katika mazingira magumu,tukafuatilia na kugundua ni kweli,hivyo tukaona tumsaidie",anasema mkurugenzi huyo wa shule.
Mzazi wa mwanafunzi huyo, Respicius Benedicto,mkazi wa mtaa wa Kashai manispaa ya Bukoba amemweleza mwandishi wa habari hii kuwa ni kweli hakuwahi kumchangia fedha yoyote ya chakula shuleni,jambo lililomfanya mwanaye kuanza kukataa shule akijificha vichakani au kuzurura mitaani,akirudi jioni sana na kuingia ndani kupitia mlango wa nyuma kwa kujifichaficha.
"Nafanya kazi ya kibarua,malipo yenyewe kiduchu,ninaye mke watoto watano,kiukweli sikumchangia mwanangu na hii inaniuma sana,ila nawashukuru waliokubali kumchukua mwanangu" amesema Benedicto
Hata hivyo habari ambazo hazikuweza kuthibitika ni kuwa pia mwanafunzi huyo alikuwa akiogopa kila akimwona mwalimu ameshika kibokò.
Mmoja wa viongozi wa shule ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji,alisema shule yake inayo mazingira mazuri ya kujifunzia yanayofuata taratibu na miongozo ya elimu katika kuchochea ujifunzaji kuanzia darasa la awali.
Wataalam wanasema watoto wanaoishi katika mazingira magumu,hasa yenye uhaba wa chakula wanakuwa na mwanzo mgumu katika ujifunzaji wa awali, na pia kuteteresha afya zao na hivyo kuathiri makuzi yao na mustakabali wa maisha yao.
Wataalam hao wanahimizwa ufanyike uwekezaji mkubwa kwa watoto wa miaka 0-8 ambacho ni kipindi muhimu cha malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Mwaka 2021 Uandikishaji nchini madarasa ya awali ulikuwa wanafunzi 1,198,564(wav.604,995 na was.593,569) huku baadhi wakitajwa kuishia njiani kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo umaskini katika familia,au mazingira yasiyo rafiki katika ujifunzaji.
Mtaalam wa sayansi ya elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya mtoto(MMMAM)kutoka shirika la Children in Crossfire-Tanzania ,Davis Gisuka,anasema kuwa darasa la awali kitaalam ni darasa la kumwandaa mtoto ili aingie darasa la kwanza,na kuwa ili mtoto huyo apate maandalizi mazuri anahitaji mazingira chanya.
"Mazingira chanya ni pamoja na mwalimu,miundombinu ya shule na uongozi kwa ujumla",anasema Gisuka,huku akimshauri mzazi wa mtoto aliyepelekwa bweni,kumtembelea mara kwa mara mwanaye ili ajisikie anapendwa na familia yake.
No comments:
Post a Comment