BARRICK BULYANHULU NA HALMASHAURI YA WILAYA YA NYANG’HWALE WASAINI MKATABA NA MAFUNDI WATAKAOTEKELEZA MIRADI YA FEDHA ZA UWAJIBIKAJI KWA JAMII - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 21 February 2023

BARRICK BULYANHULU NA HALMASHAURI YA WILAYA YA NYANG’HWALE WASAINI MKATABA NA MAFUNDI WATAKAOTEKELEZA MIRADI YA FEDHA ZA UWAJIBIKAJI KWA JAMII


Wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla hiyo
Picha ya watendaji wa Serikali wilayani Nyang’hwale na Maofisa wa Barrick Bulyanhulu


Nyang’hwale: Katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na fedha za uwajibikaji kwa jamii kutoka Mgodi wa Barrick Bulyanhulu inafanyika kwa ufanisi,viwango na kumalizika katika kipindi cha muda uliopangwa, Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale iliyopo mkoani Geita na Barrick, zimesaini mkataba wa kisheria na mafundi wanaotekeleza miradi mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2023 yenye thamani ya shilingi milioni 989,000,000/-


Hafla ya kusaini mikataba ya kisheria na mafundi wanaotekeleza miradi hiyo ilifanyika katika ofisi za Halmashauri ya Nyang’hwale na kuhudhuriwa na viongozi wa halmashauri hiyo,wananchi na wafanyakazi wa kampuni ya Barrick Bulyanhulu.


Akiongea katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyang’hwale, John Isaac John, aliwaasa washiriki wote wanaopaswa kusimamia miradi hiyo kutekeleza majukumu yao kwa umakini na weredi ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa ya viwango vya juu na inamalizika katika muda uliopangwa na mafundi kuhakikisha wanasimamia mikataba waliyoingia.


Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale ,Bi. Husna Toni,aliwaasa mafundi, walioingia mkataba na halmashauri hiyo kuhakikisha wanatekeleza kazi zao vizuri chini ya usimamizi wa wataalamu mbalimbali walioajiriwa na Serikali ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika vizuri na kuepuka kusababisha hasara ya matumuzi mabaya ya fedha hizi za CSR kufanikisha miradi ya kijamii sambamba na kuleta maendeleo kwa Wananchi.


Mwakilishi wa Meneja wa Mgodi wa Bulyanhulu, Zuwena Senkondo, katika hafla hiyo alisema kuwa Mgodi unafarijika unapokuta fedha zilizotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi zinatumika kwa lengo lililokusudiwa sambamba na kuhakikisha miradi iliyokusudiwa imejengwa kwa thamani halisi na kwa viwango vya hali ya juu “Nawaasa wadau wote tunaoshirikiana kuhakikisha fedha hizi zinakamilisha miradi yenye viwango kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.


Senkondo, aliwataka mafundi ambao wanaendesha miradi hii kuhakikisha wanawasilisha nyaraka sahihi zinazokubalika kisheria mgodini wakati wa kudai malipo yao mgodini na kuhakikisha wanalipa kodi za Serikali wanazopaswa kulipa “Sisi kwa upande wetu tukipokea nyaraka sahihi zinazokidhi vigezo vinavyotakiwa tunafanya malipo katika kipindi cha muda mfupi kuhakikisha hatukwamishi miradi kwa namna yoyote ile” alisema.


Hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano wa utekelezaji wa miradi hiyo baina ya mgodi wa Barrick Bulyanhulu na Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Meneja wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare, alisema mwaka huu mgodi huo unatarajia kuzalisha karibia wakia 215,000 za dhahabu ambapo kutokana na uzalishaji huu utatenga shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya miradi ya uwajibikaji kwa jamii iliyopendeekzwa na wilaya husika ambapo kati ya fedha hizi zitaenda kwa wilaya za Nyang’hwale na Msalala.


Baadhi ya maradi itakayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii za Barrick Bulyanhulu katika halmashauri ya Nyang’hwale katika kipindi cha mwaka huu ni kumalizia ujenzi wa wodi maalum katika hospitali ya Nyang’hwale (97,860,500/-),kumalizia ujenzi wa gereji katika kijiji cha Kharumwa (40,000,000),kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Ikangala (11,625,000),kumalizia ujenzi wa vyumba vitatu katika shule ya msingi Samia Suluhu (18,833,000),ujenzi wa choo na sehemu maalum ya kuchoma taka katika zahanati ya Iyenze (14,279,250),kukamilisha ujenzi wa jengo la maabara katika sekondari ya Mwingiro (16,000,000),kumalizia jengo la utawala katika sekondari ya Kaboha (67,602,000),kukamilisha ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya msingi ya Kharumwa (60,000,000) na kukamilisha ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa katika shule za msingi za Nyamikonze, Ngwasabuka,Iyenze na Kafita 62,500,000).


Miradi mingine ni kukamilisha jengo la utawala,maabara choo na mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Nyamtukuza (51,169,200),ujenzi wa kituo cha mabasi katika kijiji cha Ikangala (170,000,000),kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Mwingiro (74,178,450),kukamilisha ujenzi wa jengo la dharura hospitali ya Mwingiro (69,250,000),kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Nyijundu (45,885,000),mpango wa kuinua ufaulu wa wanafunzi mashuleni (25,000,000),matenki ya kuhifadhi maji na kujenga mfumo wa kuvuna maji ya mvua katia sekondari ya Mwingiro (6,000,000),ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya msingi ya Kharumwa (60,086,225),kukamilisha ujenzi wa kituo cha polisi cha Kharumwa (17,931,375) na kununua jenereta kubwa na kuimarisha miundombinu ya hospitali ya wilaya ya Nyang’hwale (50,000,000).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso