Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewatoza faini ya Sh61milioni wasambazaji saba wa kemikali aina ya Cyanide kwa makosa ya kuuza kemikali hiyo kinyume na bei elekezi iliyotolewana serikali huku wengine wakibainika kuuza kwa watu ambao hawajasajiliwa.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Januari 19, 2023 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo akizungumza kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, amesema wasambazaji hao wamebainika baada ya kikao cha Januari saba kilichotaka wasambazaji wasio waaminifu wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua.
Amesema mbali na wasambazaji kuuza kwa bei ya juu kinyume na maelekezo ya Serikali, pia wamebaini wasambazaji wanauza kwa masharti kwakuwalazimisha wale wanaotaka bei elekezi ya Sh600,000 kununua na bidhaa nyingine kama Carbon kinyume cha utaratibu na wale wanaopinga wanauziwa kwa Sh900,000 hadi Sh1.2 milioni.A
Amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Madini iliunda timu maalumu ambayo ilitembelea mikoa ya Geita, Mwanza, Mara na Shinyanga na kubaini uwepo wa mapipa 4,423 sawa na tani 221.15.
No comments:
Post a Comment