Wakazi wa Kata ya Kolandoto Manispaa Ya shinyanga Mkoani Shinyanga wameeleza adha ya ubovu wa barabara inayounganisha barabara kuu na kolandoto iliosababishwa na vifusi vilivyomwaga katikati ya barabara hiyo hali inayopelekea ajali za bajaji na pikipiki hasa nyakati za mvua.
NA HALIMA KHOYA-SHINYANGA
Wakizungumza na Kalungwa Tv Blog Desemba 31 mwaka huu ambapo wamesema vifusi hivyo vina takribani mwezi mmoja tangu kumwaga kwake.
Akieleza uhalisia wa barabara ulivyo,Alfonce Paul, amesema kuwa kumekua na changamoto kubwa pale wanapotaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine ambapo amesema upande wa usafiri imekua ni hatarishi kwa afya baada ya kuwepo kwa sehemu ndogo ya barabara inayotumika hali inayopelekea ajali.
Kwa upande wake mhanga wa ajali katika barabara hiyo,Bundala Kishiba,ambaye amevunjika mguu kutokana na kuteleza akiwa anapishana na baiskeli hali iliyopelekea kuvunjika mguu na majeraha katika mwili wake.
"Ilikuwa tarehe 13 nilikuwa natembea nateremka kwenda nyumbani nikakutana na baiskeli ikabidi nipande juu ya kifusi ili kumpisha apite lakini niliteleza na kuanguka nikavunjika mguu papo hapo, Naiomba serikali itizame changamoto hii kwakweli inatuumiza sana"Amesema Bundala.
Nao baadhi ya waendesha Bajaji wamesema vifusi hivyo vimekua ni kikwazo kikubwa kwao huku wakibainisha kuwa wamekua wakianguka mara nyingi kutokana na ufinyu wa barabara hivyo kupoteza mali zao.
Awali Katibu wa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda,Saidi Hamisi Amesema wamekuwa wakipakia wagonjwa na abiria kutoka sehemu mbalimbali huku akieleza kuwa wamekuwa wakipata lawama nyingi kutoka kwa wagonjwa wasiojiweza kutokana na kurushwa rushwa na kusumbuliwa wawapo katika pikipiki zao.
"Changamoto ya barabara inatusumbua sana kwenye mpishano wa magari,na sijui ni kitu gani kinachosababisha hadi kufikia sasa ivi bado hawajakamilisha barabara,wagonjwa wanalalamika sana wanaumizwa na barabara hii mpaka ikatubidi tusambaze kidogo ili kuongeza nafasi ya mpishano lakini hata hivyo bado bajaji na bodaboda nyingi zinapata ajali haswa kipindi hiki cha mvua,Tunaiomba mamlaka husika ije walau ivisambaze hivi vifusi ili itusaidie sisi pamoja na watumiaji wengine wa barabara kuondokana na shida hii"Amesema Saidi Hamisi.
Aidha kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kolandoto Mussa Juma,Amesema mkandarasi aliyekabidhiwa kutengeneza barabara hiyo amepata hitilafu katika mitambo yake ambayo imeharibika huku akibainisha kuwa hivi karibuni barabara hiyo itakamilika.
Awali Diwani Mussa Juma,amesema yupo karibu na wananchi ili kujua changamoto zinazo wasibu na kuahidi kua yupo katika taratibu za kumfuatilia mkandarasi wa barabara ili kukamilisha ujenzi huo.
"Mpango uliopo ni mkandarasi aliyechukua enda ya kukarabati barabara hiyo amepata changamoto ya kuharibikiwa na mitambo yake,saivi nipo mjini namfuatilia ili kuhakikisha alichokua ameniambia kwenye simu kama ni kweli,Mkandarasi amenihakikishia ndani ya siku chache atakua amekwisha kamilisha ujenzi huo"Amesema Mussa.
No comments:
Post a Comment