WAKULIMA WALALAMIKIA KUTOKULIPWA FEDHA ZA KAHAWA, WAZIRI BASHE AAGIZA KUKAMATWA VIONGOZI WA CHAMA CHA MSINGI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 6 January 2023

WAKULIMA WALALAMIKIA KUTOKULIPWA FEDHA ZA KAHAWA, WAZIRI BASHE AAGIZA KUKAMATWA VIONGOZI WA CHAMA CHA MSINGI


Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kukamatwa kwa viongozi chama cha msingi cha ushirika cha zao la kahawa cha Isaso baada wakulima kulalamika kutolipwa fedha zao licha ya kahawa yao kuuzwa.


Bashe aliyekuwa akiendelea na ziara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, msafara wake ulisimamishwa na wakulima wa kijiji cha Isansa wilayani Mbozi ambao walimueleza changamoto hiyo ya kutopewa fedha zao.


Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole alianza kwa kumweleza Bashe kuwa Amcos hiyo imekuwa ni mateso kwa wakulima kwa kushindwa kuwalipa fedha zao kwa wakati.


“Nikuombe Waziri Bashe, hawa wakulima ni masikini hawana lolote la kufanya, wamepima kahawa yao, imeuzwa hadi sasa hawajalipwa hawajui wataishi vipi, hebu tusaidie,” alisema Mwenisongole.


Katibu wa chama hicho cha ushirika, Sued Mgalla alipohojiwa na Waziri Bashe kama kahawa ya wakulima hao imeuzwa alijibu imeuzwa na fedha zipo benki.


Sued alisema fedha walizopata kwa kuuza kahawa ya wakulima hao zilikuwa benki kwa sababu bado walikuwa wanafanya mahesabu na ukaguzi wa madeni ya wakulima.


Bashe aliagiza polisi wamkamate kiongozi huyo pamoja na wenzake ili waweze kwenda kutoa fedha za wakulima walizodai zipo benki.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso