WAKAZI MSUMBIJI KOLANDOTO WALIA NA CHANGAMOTO YA MAJI,TUNAKUNYWA MAJI YENYE WADUDU,SHINYANGA. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 9 January 2023

WAKAZI MSUMBIJI KOLANDOTO WALIA NA CHANGAMOTO YA MAJI,TUNAKUNYWA MAJI YENYE WADUDU,SHINYANGA.

Wakazi wa kitongoji cha Msumbiji Kijiji cha Mwamagunguli Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga wameiomba serikali na mamlaka ya maji Mkoani humo (SHUWASA) kutatua changamoto ya uhaba wa maji ili kuondokana na adha ya kunywa maji pamoja na wanyama hali inayohatarisha afya zao.

Dimbwi la maji wanayotumia wakazi wa kitongoji cha Msumbiji Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga.


NA HALIMA KHOYA, Huheso Digital SHINYANGA.


Huheso Digital Blog imefika katika kijiji hicho hivi karibuni ambapo imefanikiwa kuzungumza na uongozi pamoja na wanakijiji wa eneo hilo na kueleza changamoto zinazowakabili.


Akieleza Adha wanazokumbana nazo wanawake katika Kitongoji Hicho,Prisca Masunga,amesema wakati wa kiangazi wanatembea umbali mrefu kutafuta maji katika madimbwi huku wakisema kuwa katika kijiji hicho kuna vikongwe ambao hawawezi kutembea umbali huo kwa ajili ya kutafuta maji hayo.


Prisca Masunga,amesema maji wanayotumia kwa sasa yanawadudu wanaoonekana na wasioonekana ambapo wanatumia maji pamoja na wanyama hali inayohatarisha afya na usalama wa wakazi hao huku wanatumia njia ya kuchemsha na kuchuja maji ili kuua vijidudu hivyo.


"Changamoto ni nyingi ikiwemo uhaba wa maji safi,maji tunayafuata mbali sana ambapo kuna vikongwe ambao hawawezi kutembea kwaajili ya kufuata maji hayo,inawabidi wanywe maji machafu ambayo yanatumiwa na wanyama yakiwa na harufu mbaya na wadudu pia,Tunaiomba serikali ituangalie afya zetu zipo hatarini sana"Amesema Prisca.


Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji hicho,Mashishanga Mayunga,Amesema katika kitongoji hicho maji hayapatikani kabisa na kwamba wanatumia maji yanayotuama katika visima pale inaponyesha mvua au kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.


Aidha Mayunga amesema maji hayo hutumiwa na wanyama wengine(Ng'ombe,mbuzi na kondoo) huku yakiwa na wadudu wanao onekana na wasio onekana hali inayohatarisha afya zao.


"Hatuna maji ya kunywa inapelekea kuchangia maji na wanyama,wakati wa kiangazi tunahangaika sana kuna wabibi wengine wanashindwa kwenda umbali mrefu kutafuta maji,hivyo tunaiomba mamlaka husika iweze kusikia kilio chetu"Amesema Mayunga.


Aidha kwa upande wake,Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji,Ikandi Ngassa Nkuzinza,amesema awali kwenye kijiji hicho walikuwa wanatumia maji ya kisima cha kina kirefu walichounganishwa na Mradi wa kuongeza maji ambapo bomba la kisima hicho lilikatika katika mto wa Mwamagunguli hali iliyopelekea kitongoji cha msumbiji kukosa huduma hiyo.


Ngassa,ameiomba mamlaka ya maji safi na salama Mkoa Shinyanga,SHUWASA kuwasaidia walau maji yatokayo mwanza ili kuepuka adha wanazokumbana nazo vipindi vyote vya Mwaka.


Akieleza mpango mkakati wa mamlaka ya maji safi na salama Mkoa Shinyanga SHUWASA,Kaimu mkurugenzi,Mwandumbia Ruben,amesema wakazi hao wa Msumbiji walikuwa wanatumia maji ya kisima ambacho kilipata hitilafu katika mto wa mwamagunguli huku akibainisha kuwa kitongoji hicho kipo katika orodha ya sehemu zitakazo pata maji hivi karibuni.


Ruben,Amewaasa wananchi wa kitongoji hicho kuwa wavumilivu katika kipindi hichi ambacho mamlaka ya maji iko katika hatua za awali kwaajili ya kuwafikishia huduma ya maji.


Mashishanga Mayunga mkazi wa kitongoji cha Msumbiji Kata ya Kolandoto akieleza adha wanayokutana nayo kwa kunywa maji machafu yenye wadudu.


Rukia,Mkazi wa Kitongoji cha msumbiji akieleza namna wanavyotembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye madimbwi na visima Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso