KONGAMANO LA BIASHARA KULETA KAMPUNI 400 TANZANIA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 24 January 2023

KONGAMANO LA BIASHARA KULETA KAMPUNI 400 TANZANIA

KAMPUNI 400 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) zinatarajia kuja nchini mwezi ujao kwa ajili ya kuangalia fursa za uwekezaji na biashara kupitia kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika Februari 23 na 24 mwaka huu, Dar es Salaam.


Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Manfredo Fanti alisema hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.


Balozi Fanti alisema EU ni mshirika mkubwa wa biashara na uwekezaji wa Tanzania ambapo katika kipindi cha mwaka 2021, kiwango cha thamani ya biashara ya EU kwa Tanzania ilikuwa Euro milioni 856 na thamani ya biashara ya Tanzania kwa EU ilikuwa Euro milioni 456.


Alisema katika kipindi cha mwaka 2020, thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (DFI) kutoka kwa kampuni za nchi kumi hai zaidi wanachama wa EU hapa nchini ulikuwa Dola za Marekani bilioni 1.5 kati ya mwaka 2013 na 2020.


“Utafiti uliofanywa mwaka 2021 kwa kampuni takribani 100 za Umoja wa Ulaya zilizoanzishwa hapa ulionesha kuwa wana hisa kwa pamoja za uwekezaji wa takribani Euro milioni 685, lakini tunaamini kuwa Tanzania ina fursa kubwa zaidi za uwekezaji kama inavyothibitishwa na mipango ya kampuni zilizofanyiwa utafiti kuwekeza Euro zaidi ya milioni 250 katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema Balozi Fanti.


Alisema kampuni hizo 400 ni miongoni mwa nyingi za Ulaya zilizoonesha nia ya kutaka kuwekeza na kufanya biashara Tanzania.


Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah, Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Mifumo ya Taarifa wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mafutah Bunini, alisema kongamano hilo la biashara ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.


Bunini alisema EU ni mdau muhimu wa biashara na uwekezaji wa Tanzania na ndiyo maana kampuni 400 kutoka nchi hizo za Ulaya zimethibitisha kuja kushiriki kongamano hilo ambalo litapanua soko la bidhaa za Tanzania katika soko la Ulaya.


“Tanzania bado hatujalifikia soko la Umoja wa Ulaya kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wao wanavyolifikia soko letu, hivyo nitoe wito kwa Watanzania kutumia fursa hii kuanzisha ushirikiano na ubia na kampuni zitakazokuja ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta za kilimo, viwanda, madini, teknolojia, nishati na nyinginezo, TIC tutahakikisha mpango huu unafanikiwa,” alisisitiza Bunini.


Mkuu wa Idara ya Ushirikiano ya EU, Cedric Merel, alisema kufanyika kwa kongamano hilo ni kuitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutaka wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza Tanzania.


Merel alisema kongamano hilo litatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wenzao kutoka nchi 27 wanachama wa EU.


Mkuu wa Idara ya Utawala na Uchumi wa EU, Karina Dzialowska, alisema wanatiwa moyo na msukumo wa Serikali ya Tanzania katika kuvutia biashara na uwekezaji nchini.


Kwa mujibu wa EU, kampuni 200 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zinatarajiwa kushiriki kongamano hilo na kufanya kampuni zote zitakazoshiriki kuwa 600.


CHANZO:HABARILEO.CO.TZ

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso