DED ALALAMIKIWA KUKAA MBALI NA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 25 January 2023

DED ALALAMIKIWA KUKAA MBALI NA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)


Na Mwandishi Wetu, Iringa

MKURUGENZI wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bashir Muhoja amekalia kuti kavu baada ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Iringa kutangaza kutokuwa na imani naye.


Katika kikao cha halmashauri ya chama hicho kilichofanyika leo mjini Iringa, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Constantino Kiwele amesema mtendaji huyo hana mahusiano mazuri na chama na hivyo kuathiri ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani yao.


Akimshitaki mkurugenzi huyo kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (MNEC), Salim Asas, Kiwele almesema; “Tunaleta malalamiko hayo kwenu ili mchukue hatua zikazosaidia kunusuru yanayoendelea.”

Akizungumzia zaidi pengo la mahusiano hayo Kiwele amesema hakumbuki ni lini mkurugenzi huyo alipokea simu yake au kumpigia ili kwa pamoja wazungumzie utekelezaji wa Ilani.


Diwani wa kata ya Ilolompya, Fundi Mihayo alisema wanapitia katika kipindi kigumu katika kufanya kazi na mtendaji huyo wa halmashauri na akaomba kilichozungumzwa na mwenyekiti wa CCM kifanyiwe kazi.


Mkurugenzi huyo hakuwepo kwenye kikao na alipopigiwa simu kupatikana kuzungumzia madai hayo na taarifa kutoka kwa mmoja wa wasaidizi wake inaonesha yupo Dodoma kikazi.


Akipokea malalamiko hayo MNEC Asas ameahidi kuyafikisha katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa ambayo moja ya wajumbe wake ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa.


Asas alikumbusha umuhimu wa watendaji wa serikali kushirikiana na chama hicho akisema wakati fulani makosa yao ya kiutendaji yamekuwa yakikisababishia chama chao lawama kubwa toka kwa wananchi na washindani wao wa kisiasa.


“Yaani unawezakuta kosa linafanywa na Mkurugenzi au mtendaji fulani lakini lawama zinakuja kwetu kwasababu sisi ndio tumeunda hii serikali. Na badala ya watendaji hao kushukuru wakati fulani kwa kuwatetea, malipo yake ni kutotaka kushirikiana na sisi,” amesema.


Wakati huo huo Asas ameitaka halmashauri hiyo kushirikiana na wana CCM wenzao kuhakikisha wanafanya kazi itakayokibakisha chama chao madarakani, kuendelea kukiimarisha chama hicho na kuisemea serikali kwa kazi zote inazofanya.


Aidha ameahidi kuipa CCM wilaya hiyo msaada wa kifedha ili iweze kukamilisha mradi wake wa ujenzi wa milango ya biashara pembezoni mwa ofisi zake itakayokuwa moja ya vyanzo vyake vya mapato.


Katika kujiimarisha zaidi kiuchumi ameshauri chama hicho katika ngazi mbalimbali kujikita katika kilimo cha miti na parachichi akisema, sekta hiyo inaweza kuzalisha mapato ya uhakika kama ikisimamiwa ipasavyo.


CHANZO:FULLSHANGWE

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso