Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuanzia Januari 01, 2023 limefanya misako na doria zenye tija kukabiliana na vitendo vya uhalifu na wahalifu na kuhakikisha wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu. Katika kipindi hicho, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali 165 yakiwemo wizi kwa njia ya mtandao, kupatikana na nishati ya mafuta isivyo halali, kubaka, wizi wa pikipiki, kupatikana na bidhaa za magendo, kupatikana na pombe ya moshi na kupatikana na kiwanda bubu cha kutengeneza pombe kali.
MTUHUMIWA MMOJA ANASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA WIZI KWA NJIA YA MTANDAO.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JOHN SHAGAMA [25] Mkazi wa Ludewa/Sengerema Mwanza ambaye anatuhumiwa kuhusika katika matukio manne ya kuiba fedha kwa njia ya mtandao.
Mtuhumiwa amekuwa akitumia namba tofauti tofauti za mitandao ya simu kuwalaghai na kuwatapeli fedha mawakala wa huduma za kifedha kwa kufika maeneo yao ya biashara huku akijidai hana simu hivyo kuomba apewe simu ya wakala kwa ajili ya kutuma fedha kwa mtu mwingine na badala yake huingia kwenye orodha ya majina yaliyopo kwenye simu hiyo na kubadilisha baadhi ya namba kwa kuweka namba zake kwa majina aliyoyakuta humo.
Baada ya kufanya hivyo uondoka na badae kupiga simu kwa wakala kuomba atumiwe kiasi fulani cha fedha wakati huo wakala akijua anatuma fedha kwa mteja wake au mwajiri wake (boss) kumbe anatapeliwa.
Mtuhumiwa amekutwa na simu 05 za mkononi pamoja na laini 13 ambazo hutumia kulaghai, kutapeli na kuiba fedha. Baada ya mahojiano mtuhumiwa amekiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya wizi kwa njia ya mtandao maeneo ya Mbeya mjini, Mkoa wa Songwe, Tabora Wilaya ya Uyui, Njombe, Mwanza, na Dar es salaam.
WASHIKILIWA KWA KUPATIKANA NA KIWANDA BUBU CHA KUTENGENEZA KONYAGI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maofisa toka Kampuni ya TDL (Tanzania Distillers Limited) ya Jijini Dar-es-Salaam linawashikilia 1. YUSUPH GEORGE NJAMASI [38] Mkazi wa Ituha na 2. FRANK DAVID KASEKE [34] Mkazi wa Itezi Gombe kaskazini kwa tuhuma za kupatikana na kiwanda bubu cha kutengeneza pombe kali kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa na mwenzake walikamatwa wakiwa kwenye nyumba waliyopanga inayomilikiwa na ROBERT BANTU huko maeneo ya Ituha Jijini Mbeya wakiwa na Kiwanda Bubu cha kutengenezea Pombe kali na kisha kujaza kwenye chupa zenye lebo za viwanda halali vya kutengneza pombe kali hapa nchini. Watuhumiwa walipekuliwa na kukutwa na vifaa mbalimbali:-
Stika zenye nembo za vinywaji vikali,
Boksi 04 za mifuko,
Kifungashio kimoja chenye stika za TRA,
Dumu moja la Spirit lenye ujazo wa lita 250,
Dumu tupu 16 zenye ujazo wa lita 250
Ndoo 01 yenye ujazo wa lita 20 ikiwa na spiriti ya kutengenezea vinywaji vikali
Diaba moja lenye ujazo wa lita 120 likiwa tayari na pombe kali iliyotengnezwa ikisubili kujazwa kwenye chupa,
Mifuko ya sandarusi 36 ikiwa na chupa tupu za pombe kali,
Freva ya pombe kali mbalimbali,
Mifuko ya sandarusi 12 ikiwa na Maboksi tupu ya kuwekea pombe kali.
Watuhumiwa wanajihusisha na viwanda bubu vya kutengenezea vinywaji vikali bandia zisizo na ubora. Ufuatiliaji unaendelea kubaini na kukamata mtandao wa wahusika wote. Tunatoa wito kwa wamiliki wa viwanda vinavyotengeneza vinywaji mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutambua vinywaji halali na bandia.
WATUHUMIWA WATATU WANASHIKILIWA KWA KUPATIKANA NA NISHATI YA MAFUTA ISIVYO HALALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na misako na doria kuzunguka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ambapo huko maeneo ya Kijiji cha Ilongo, Kata ya Mahongole, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu ambao ni CREVA MUSA [19] Mkazi wa Ruaha Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe, ANORLD ZABRON [23] Mkazi wa Kigoe Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe na AWADI MOSES [28] Mkazi wa Mwatenga Mbarali Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nishati ya mafuta aina ya Diesel ujazo wa lita 240 pamoja na madumu tupu 09 isivyo.
halali. Watuhumiwa ni wezi na wauzaji haramu wa nishati ya mafuta, watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
AFUNGWA JELA MAISHA KWA KOSA LA KUBAKA MTOTO.
Mshitakiwa ISAYA LATSON [23] Mkazi wa Chalangwa Wilaya ya Chunya amehukumiwa kwenda jela kifungo cha maisha na mahakama ya Wilaya ya Chunya baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumbaka mtoto jina tunalihifadhi mwenye umri wa miaka minne Mkazi wa Chalangwa Wilaya ya Chunya.
Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 11/2023 imetolewa tarehe 24/01/2023 chini ya kifungu 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka 2022 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya Mhe. JAMES JULIUS MHANUSI…SRM mbele ya mwendesha mashitaka wa serikali MAZOYA LUCHAGULA….
Ni kwamba mnamo tarehe 21.01.2023 majira ya saa 02:08 usiku huko Kijiji na Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mshitakiwa ISAYA LATSON [23] alimdanganya mtoto huyo kuwa anaenda kumnunulia Soda dukani badala yake akaenda nae kwenye korongo na kumbaka kwa nguvu kitendo kilichomsababishia maumivu makali.
Hata hivyo, mtuhumiwa alijitetea kwa kuomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa alitenda kosa hilo kutokana na tamaa za mwili na ulevi. Mahakama imetupilia mbali utetezi huo ili iwe fundisho kwa wengine.
ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA WIZI WA PIKIPIKI.
Kufuatia misako na doria iliyofanyika kati ya Januari 22 hadi 23 huko maeneo ya Kijiji na Kata ya Isuto, Tarafa ya Iwindi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kumkamata TATIZO POSTA [22] Mkazi wa Isuto akiwa na Pikpiki MC 315 CKY aina ya Kinglion aliyoiiba kwa VESTIN RAPHAEL ambapo alitaka kuitorosha kuipeleka Mkoa wa Songwe Wilaya ya Mbozi. Upelelezi ukikamilika atapelekwa mahakamani.
WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUVUNJA NYUMBA USIKU NA KUIBA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia ALEX MGIMBA [13] Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kalobe Kidato cha Pili na CHRIS FRANK [16] Mkazi wa Kalobe kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya kuvunja nyumba nyakati za usiku na kuiba.
Watuhumiwa walikutwa na Fremu nne za madirisha ya Aluminium ambazo ni mali za wizi. Aidha wamehojiwa na kukiri kuhusika katika tukio la kuvunja nyumba usiku tarehe 24/12/2022 huko maeneo ya Kalobe Jijini Mbeya.
WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia AUGUSTINO MNYEKE [50] Mkazi wa Vwawa Mbozi Mkoa wa Songwe, REGINARD MWINYI [22] Mkazi wa TEKU, ALEX JOSEPH [27] Mkazi wa Ilolo, GASPA AMOS [17] Mkazi wa Kiwira, ALPHONCE MACRINE [27] Mkazi wa Ilongoboto na LENARD WILLIAM [20] Mkazi wa Soweto kwa tuhuma ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi Kilo 67 na Gramu 137.5 pamoja na mbegu za bhangi zenye uzito wa Gramu 260.
Watuhumiwa walikamatwa katika misako iliyofanyika Mtaa wa Halengo, Sterio na Mabanzini Jijini Mbeya na Kasumulu Wilaya ya Kyela. Watuhumiwa ni wauzaji wa dawa hizo za kulevya, watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA MALI ZA MAGENDO NA BIDHAA ZILIZOPIGWA MARUFUKU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa 1. REHEMA ANYIMIKE [27] Mkazi wa Mbugani na 2. CHIEF CHRISTIAN [33] wakiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku nchini aina ya A1 Gin chupa 27, WIN chupa 13.
Aidha watuhumiwa IBRAHIM EZRON MWAITEKE [41], TAIFA JACKSON ELIUS [24], LUCAS PAULO SAMSON [23] na JORO SAID MWAKAJINGA [40] walikamatwa wakiwa na Boksi 112 za Mayai ya kuku wa kisasa yanayokadiriwa kuwa na thamani ya 2,500,000/= wakiingiza nchini bila kulipia ushuru wa forodha baada ya kuyavusha kupitia vivuko visivyo rasmi kutokea nchi jirani ya Malawi na kuyasafirisha kwa Gari namba T.714 DLE Toyota Coaster.
Sambamba na hilo, Januari 02, 2023 huko Wilaya ya Mbeya Vijijini tulifanikiwa kukamata gari T.948 ASL Toyota Mark X rangi ya Silver ambayo baada ya kufanya upekuzi tulikuta vitenge jola 79 sawa na doti 474, vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini ambavyo ni Princess Clair pc 6, Extra Clair pc 72, Extra Clair Lemon pc 18, Betasol dazan 20 na Epiderm pc 30.
Aidha katika misako hiyo Pombe haramu ya Moshi [Gongo] ujazo wa lita 366 na Mitambo miwili ya kutengenezea Gongo na Pikipiki MC 449 BSH aina ya Boxer ilikamatwa, mali za wizi vitenge doti 38 vikisafirishwa kwenye Gari T.948 ASL Toyota Mark X rangi nyeupe zilikamatwa. Pikipiki tatu mali za wizi zilikamatwa, watuhumiwa wa matukio ya mauaji 19 kati yao wanaume 16 na wanawake 03 akiwemo mama aliyemuua mtoto wake huko Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za wizi wa fedha wamekamatwa.
Taarifa ya ukamataji wa makosa na madeni ya usalama barabarani mkoa wa Mbeya kuanzia tarehe 01/01/2023 hadi tarehe 24/01/2023.
Jumla ya makosa yote yaliyokamatwa ni 7085 ambapo idadi ya magari ni 5336 sawa na idadi ya Pikipiki ni 1749. Aidha jumla ya magari yaliyokamatwa yakidaiwa madeni ni 2160. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria n ahata ajali zinazoweza kuepukika.
WITO: Kamanda wa Polisi Mkoa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi BENJAMIN KUZAGA anatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwani kwa Mkoa wa Mbeya havina nafasi badala yake kufanya kazi halali za kujipatia kipato. Aidha anatoa wito kwa wazazi kuongeza umakini katika ulinzi na kuwalea watoto ili kuwaepusha na vitendo vya kikatili kama vile ubakaji, ulawiti na vingine.
Imetolewa na
Benjamin E. Kuzaga – ACP
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya.
“Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu…Msingi wa Mafanikio Yetu”
No comments:
Post a Comment