KIKUNDI cha Umoja wa Hisa endelevu Kanyigo(UHIKA) kilichoko kata ya Kanyigo,wilayani Missenyi, kimepongezwa kwa jinsi kinavyojitoa katika kuguswa na masuala ya kijamii ikiwemo kuchangia wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi katika shule za serikali katani humo.
Na Mutayoba Arbogast, Huheso Digital Bukoba
Pongezi hizo zimetolewa jana na Kaimu Afisa tarafa wa tarafa Kiziba,Muanuzi Josephati katika sherehe ya uzinduzi rasmi wa mradi wa nyumba ya kulala wageni,unaoendeshwa na UHIKA.
Kwa mujibu wa Theonest Kashunja, Mwenyekiti wa umoja huo ambaye pia ndiye Mkurugezi wa mradi wa nyumba ya wageni iitwayo Mikimba Galaxy,waliamua kuingia mkataba na mmiliki wa nyumba hiyo mwaka mmoja uliopita,ikiwa ni moja ya mikakati ya miradi kadhaa wanayomiliki,ili asilimia 30 ya faida watakayopata,iweze kuwasaidia wanafunzi wanaochukua masomo ya Sayansi katika shule mbili za serikali za Kikukwe na Kigarama,zilizopo katani humo.
Kwamba mwaka 2018 walitoa msaada kidogo kwa shule mojawapo,lakini wakaona katika kupanua wigo wa utoaji msaada kwa wanafuzi wa Sayansi na wale wenye mazingira magumu,pamoja na motisha kwa walimu,wakaamua kuwekeza katika biashara hiyo ya nyumba ya wageni ikiwa pia inaambatana na miradi ya hoteli,mashine ya kuranda mbao nk.
Umoja huo wenye wanachama 11,ikiwa ni wanawake wawili na wanaume tisa,ulisajiliwa na Halmashauri ya wilaya ya Missenyi mwaka 2017,na kwa sasa una mtaji wa zaidi ya sh milioni 30,kutokana na kuuza hisa na na kutoka kwenye miradi yao
Pia huchangia katika mfuko wa jamii kusaidiana katika shida na raha,sambamba na kukopeshana.
Kaimu Afisa tarafa huyo,amesema ameridhishwa na kiwango cha utendaji wa viongozi na wanachama,hasa kuguswa na wanafuzi,na kuwahimiza vikundi vingine kutenda kadri ya katiba zao bila kuwa na ndoto za kujitajirisha kupitia migongo ya wanachama,bali kwa maslahi mapana ya jamii.
Jumla ya sh 456,000 imepatikana kutokana na harambee katika uzinduzi huo wenye lengo la kufanya huduma za biashara hiyo kuwa bora zaidi.
Kaimu Afisa tarafa wa tarafa Kiziba,Muanuzi Josephati katika sherehe ya uzinduzi rasmi wa mradi wa nyumba ya kulala wageni
Mradi wa nyumba ya kulala wageni,unaoendeshwa na UHIKA
No comments:
Post a Comment