SERIKALI YAPINGA SABAYA KUACHIWA HURU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 13 December 2022

SERIKALI YAPINGA SABAYA KUACHIWA HURU

Ofisi ya Mwendesha Mashitaka nchini (DPP) amekata rufaa kupinga hukumu iliyowaachia huru aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake watano



Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilipanga kuanza kusikiliza rufaa hiyo namba 155/2022 iliyokatwa na upande wa Jamhuri dhidi ya hukumu iliyotolewa na Hakimu mkazi Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha.
Mbali na Sabaya wajibu rufaa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.


Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021 iliyotolewa uamuzi na mahakama hiyo ya chini aliyekuwa mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo (Watson Mwahomange) hajajumuishwa katika rufaa hiyo


Mbele ya Jaji Salma Maghimbi, warufani wa wengine leo hawakuwepo mahakamani hapo isipokuwa Sabaya peke yake.


Kwa upande wake Sabaya, aliieleza mahakama kuwa hana mwakilishi na kuwa amepata wito wa mahakama rufaa hiyo leo akiwa gereza.


"Hata sasa hivi sijafahamu nipo kwa ajili gani hivyo sijatafuta wakili na nimetoka Moshi chini ya uangalizi wa daktari naumwa," alidai Sabaya.


Mjibu rufaa huyo aliiomba mahakama hiyo muda wa wiki mbili ili aweze kujiandaa na kufanya mawasiliano na mawakili wake pamoja na familia yake.


Baada ya maelezo hayo Jaji huyo alimweleza Sabaya kuwa rekodi zinaonyesha aliachiwa huru na Jamhuri imekata rufaa.


Akiahirisha rufaa hiyo Jaji Maghimbi alisema rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa mfululizo kwa muda wa siku tano na wakili wa mjibu rufaa wa kwanza hajasema kama haendelei kumwakilisha hivyo rufaa hiyo kuanza kusikilizwa Desemba 13.


Juni 10,2022 Sabaya na wenzake sita walishinda kesi ya uhujumu uchumi na kuachiwa huru baada ya mahakama hiyo ya chini kubaini ushahidi uliotolewa na jamhuri ulighubikwa na utata hivyo kushindwa kuthibitisha mashitaka yaliyokuwa yanawakabili na kuwatia hatiani..

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso