Mchungaji na mfanyabiashara raia wa Nigeria, Henry Ozoemena, anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 20 za dawa za kulevya aina ya Heroine, amefariki dunia baada ya kupata shambulio la moyo akiwa mahabusu katika gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Wakili Yasin ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Ijumaa Desemba 30, 2022, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Ozoemena (47) na wenzake wawili raia wa Lativia, ambao ni Linda Mazure (24) na mchumba wake Martins Plavins (23), wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 61/2021, yenye mashtaka ya kusafirisha dawa hizo za kulevya.
Mchungaji huyo alidakwa April 2019 na Jeshi la Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya katika nyumba iliyopo Mtaa wa Pemba, Kariakoo, Dar es Salaam.
Wakili wa Ozoemena, Hassan Yasin ametoa taarifa hiyo, Mahakama hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Rhoda Ngimilanga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Yasini ambaye alishika mikoba ya wakili Elipatra Ali, amedai mahakamani hapo mteja wao aliugua akiwa gereza la Segerea baada ya kupata madhara ya shambulio la moyo.
Amedai Ozoemena aliaguka wakati anatembea katika gereza hilo na alipopelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu ndio ilibainika kuwa alipata shambulio la moyo na wakati akipatiwa matibabu alifariki dunia.
Wakili huyo amedai mteja wao walifariki wiki mbili zilizopita na tayari mwili wake umesafirishwa kwenda nchini Nigeria kwa ajili ya mazishi.
Awali, Wakili wa Serikali Faraja Ngukah aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.
Ngukah baada ya kueleza hayo, wakili Yasini aliomba upande wa mashtaka kukamilisha haraka taratibu za kusajili taarifa na nyaraka muhimu Mahakama Kuu ili kesi hiyo iweze kuendelea.
"Mheshiwa hakimu, kesi hii ni ya muda mrefu na washtakiwa wapo ndani hawana dhamana, hivyo ni vyema upande wa mashtaka wakafanya haraka kusajili taarifa muhimu Mahakama Kuu ili kesi hii iweze kuendelea kwa hatua nyingine" amedai wakili Yasini
Pia, wakili Yasin ameiomba siku kesi hiyo itakapoitwa mahakamani hapo, washtakiwa wapelekwe mahakamani ili waende kuonana na kiongozi wa Waendesha Mashtaka Mahakama ya Kisutu.
Akijibu hoja hizo, wakili Ngukah amedai atahakikisha nyaraka hizo zinasajiliwa mapema iwezekanavyo ili kesi hiyo hiyo iweze kuendelea.
No comments:
Post a Comment