JESHI la Polisi mkoani Kagera limesema likiwa katika operesheni ya kuwanasa watuhumiwa wa ujambazi katika kijiji cha Muganza kata na tarafa ya Murusagamba wilayani Ngara, wamefanikiwa kuwaua majambazi watatu kati ya watano, baada ya majibizano ya risasi.
NA MUTAYOBA ARBOGAST-BUKOBA
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, ACP. William Mwampaghale,imesema kuwa watu hao wamekamatwa tarehe 15/11/2022 majira ya saa 4:30 usiku, kufuatia taarifa za kiintelejensia kuwa kuna kikundi cha majambazi kinapanga kufanya uhalifu na unyang'anyi kwa kutumia silaha.
Katika tukio hilo, polisi wamefanikiwa kukamata silaha, Bunduki aina ya AK 47 isiyokuwa na namba,na magazini moja ikiwa na risasi 12,huku watuhumiwa wawili wakifanikiwa kutoroka.
Watu hao watatu waliokamatwa wanaodhaniwa kuwa majambazi, wametajwa kuwa na umri wa miaka kuanzia 23 hadi 35, na wakati wanakimbizwa hospitali ya wilaya ya Ngara, Nyamiaga kwa matibabu, wawili walifariki dunia na majina yao hayakutambuliwa mara moja,na miili yao imehifadhiwa katika hospitali hiyo ya Nyamiaga kwa utambuzi.
Uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kikundi cha watu hao,kimekuwa kikifanya unyang'anyi wa kutumia silaha tangu Septemba 2022 katika maeneo ya kijiji cha Bugarama, Muganza na Murusagamba wakivamia wananchi kwenye biashara zao na maeneo ya barabarani,na kuwapora fedha na mali zao.
Jeshi la polisi mkoani Kagera linatoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu wa aina yoyote kuacha mara moja,na pia linawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa sahihi za uhalifu pamoja na wahalifu ili hatua za kudhibiti zichukuliwe haraka.
No comments:
Post a Comment