RASMI: JAMES MBATIA BYE BYE NCCR-MAGEUZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 2 November 2022

RASMI: JAMES MBATIA BYE BYE NCCR-MAGEUZI


Ikiwa imepita miezi mitano tangu kuibuka kwa mvutano wa makada ndani ya Chama cha NCCR Mageuzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imebariki kung’olewa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.


Mei 21, Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi iliitisha mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu Kurasini na miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na kumsimamisha James Mbatia kujihusisha na shughuli za chama.


Hata hivyo, Septemba 24, mkutano mkuu maalum wa NCCR Mageuzi uliofanyika jijini Dodoma ulimvua uanachama James Mbatia na kumfuta uongozi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Angelina Rutairwa.


Mwananchi limeiona barua iliyotoka ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa nchini na kusainiwa na Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza ikihalalalisha mabadiliko ya viongozi hao wakuu wa chama hicho kikongwe cha upinzani nchini.


Katika barua hiyo iliyoandikwa Oktoba 24, msajili ameeleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 23, 26, 28 na 31(2) ya Kanuni na Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa, vikao hivyo vya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama yalifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na katiba ya NCCR Mageuzi.


“Msajili wa Vyama vya Siasa ameridhika kuwa kikao cha halmashauri kuu ya chama chenu cha Septemba 23, kikao cha halmashauri kuu cha Septemba 24 na mkutano mkuu wa Septemba 24 uliofanya mabadiliko ya uongozi na katiba ya chama chenu yalifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyotolewa na msajili.


Akizungumza na wanahabari hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa NCCR (Bara) Joseph Selasini alisema sasa umefika wakati mtu yeyote atakayeongea na kujitambulisha kama kiongozi wa chama kinyume na utaratibu, sheria itafuata mkondo wake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso