NGEDERE WAVAMIA MASHAMBA MISSENYI, LISHE KWA WATOTO WADOGO MASHAKANI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 2 November 2022

NGEDERE WAVAMIA MASHAMBA MISSENYI, LISHE KWA WATOTO WADOGO MASHAKANI


BARAZA la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Missenyi,limejadili na kusikitishwa na hali inayoweza kutokea kuhusu uhaba wa chakula,na hivyo kudumaza lishe hasa kwa watoto wadogo chini ya miaka nane,kutokana na ngedere wanaovamia mashamba na kula mazao.



NA MUTAYOBA ARBOGAST-HUHESO DIGITAL-BUKOBA


"Nasikitika kata yangu ya Kitobo inaweza kukumbwa na baa la njaa wanyama hawa waharibifu wasipodhibitiwa,maana wametoka mwituni na kuhamia vijijini,wakila kila aina ya zao",amesema diwani wa kata ya Kitobo,Willy Mutayoba


Imeelezwa kuwa kata zilizokumbwa hasa na uvamizi wa wanyama hao ni Ruzinga,Buyango,Kitobo na Bwanjai.


Kata nyingine ni Kanyigo,Kashenye,Ishozi na Ishunju,zote za tarafa ya Kiziba na kwa kiasi fulani katika tarafa ya Missenyi.


Kwamba hali hiyo ya wanyama waharibifu isipodhibitiwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula,ikizingatiwa kuwa pia mvua zilizotarajiwa hazikunyesha inavyostahili,na hivyo mazao yaliyopandwa msimu huu yakiwemo mahindi na maharage,yamenyauka kutokana na jua kali.


"Wanyama hawa wanaharibu kila zao linalopatikana,hata kahawa mbivu shambani,na hii ni hatari",amesema diwani wa kata ya Kashenye,Domitian Nshambya



Madiwani hao wameonya kuwa waathirika wakubwa watakuwa watoto wadogo wanaohitaji lishe ya kutosha tena yenye mchanganyiko wa vyakula,na hivyo kuiomba serikali kufanya kila jitihada kuwaondoa wanyama hao, katika kuhakikisha lishe bora inaendelea kupatikana


Madiwani wa kata ya Ruzinga Rafihu Hussein na Letisia Paschal wa kata ya Kilimilile,wameonya juu ya ukataji miti holela na uharibifu wa uoto wa asili ambako ndiko makazi ya wanyama hao huku wakila matunda ya mwituni,na kwa kuwa makazi yao yameharibiwa na hawana chakula cha kutosha ndiyo maana wamelazimika kuvamia vijiji.


Afisa maliasili wa wilaya ya Missenyi, James Matekere,amesema wamejipanga kuwaondoa wanyama hao karibu na makazi ya wananchi kwa kuwafukuza bila kuwadhuru hadi makazi yao ya asili,na kuwa Halmashauri ya wilaya ya Missenyi kwa kushirikiana na wananchi,tayari wameagiza risasi na vifaa vingine kwa ajili ya kazi hiyo,zoezi litakaloanzia tarafa ya Kiziba,na kisha tarafa ya Missenyi.


Kwa mujibu Tathmini ya awali ya Uzalishaji mazao ya chakula msimu wa 2021 na Upatikanaji wa chakula 2021/2022 iliyofanywa na Wizara ya Kilimo,Matarajio ya uzalishaji mazao ya chakula mkoa wa Kagera ilikuwa mazao ya nafaka tani 257,306,na mazao yasiyo ya nafaka tani 972,960 huku matarajio ya mavuno ikiwa ni tani 1,139,154.


Ripoti ya Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM),inaonesha jitihada za kushughulikia hali ya lishe kwa watoto nchini zimekuwa za mafanikio makhbwa zikijumiisha wadau mbalimbali,ingawa mtoto mmoja kati ya kumi bado wanakabiliwa na udumavu mkali,hivyo jitihada zaidi zinahitajika.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso