Idadi ya maambukizi ya kifua kikuu imepungua kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 kufikia wagonjwa 208 kwa kila watu 100,000 mwaka 2021 ambapo ni sawa na asilimia 32.
Akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Abel Makubi leo Ijumaa Novemba 15, 2022 kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa mpango wa taifa wa kudhibiti Kifua kikuu na ukoma jijini Mwanza, Mkuu wa Programu na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya, Dk Catherine Joachim amesema hadi ifikapo mwaka 2030 Serikali kwa kushirikiana na wahudumu wa Afya, wadau na jamii inatakiwa kutokomeza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo.
“Katika kipindi hicho (2015), vifo vimeweza kupungua kutoka takribani vifo 55,000 kwa mwaka sawa na watu 150 kwa siku hadi kufikia takribani vifo 25,800 kwa mwaka 2021 ambavyo ni sawa na vifo 70 kwa siku,”amesema
Dk Catherine amewataka watoa huduma wa Afya kutumia mfumo wa Afya wa kuchukua takwimu za wagonjwa wa kifua kikuu na ukoma kieletroniki ili kuiwezesha Serikali kujua idadi halisi ya wanaopata magonjwa hayo na vifo vinavyotokea kwa kuwa takwimu za magonjwa hayo bado ni zamakadirio.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amesema licha ya kufanikiwa kwenye mapambano ya magonjwa hayo wanakabiliwa na changamoto ya ushiriki mdogo wa vituo binafsi vya kutolea huduma ya Afya na wadau.
Amesema kiwango kidogo cha uhudhuriaji wa wagonjwa wa kifua kikuu sugu nchini kinachochangiwa na kiwango kidogo cha upimaji wa sampuli za makohozi kwa njia ya vina saba pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu visababishi na dalili za magonjwa hayo.
Amesema kati ya vituo vya Afya vya binafsi takribani 2,596 vilivyopo ambavyo pia vimesajiliwa ni vituo 506 tu ambavyo ni sawa na asilimia 20 ndivyo vinatoa huduma ya upimaji wa kifua kikuu na kudai changamoto hiyo itatuliwe ili sekta binafsi nayo iongeze huduma ya mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
“Kwa mwaka huo (2022) wagonjwa 87,415 wa kifua kikuu waligunduliwa na kuwekwa kwenye matibabu ikiwa ni sawa na asilimia 65 ya makadirio ya shirika la Afya Duniani, hivyo bado tunalo jukumu la kuwapata hawa asilimia 35 ambao bado wapo katika jamii tunayoishi wakiendelea kuambukiza wengine,”amesema
“Idadi ya wagonjwa wapya wa ukoma wanaoendelea kugunduliwa nchini inaendelea kupungua mwaka mpaka mwaka, katika miongo miwili iliyopita nchi yetu imeweza kuwagundua na kuwatibu wagonjwa wapya wa ukoma zaidi ya 121,000 na kwa mwaka 2020 walikuwepo wagonjwa wapya 1,208 na idadi ya watoto waliogundulika na ukoma ni 48,”amesema
Akiwakilisha wadau wa kupambana na magonjwa hao, Muwakilishi wa Shirika la Management and Development for Health (MDH), Eric Harris ameishukuru Serikali kutoa nafasi kwa wadau wa Afya kushiriki kutekeleza mpango wa vita dhidi ya kifua kikuu na ukoma akidai wamefanikiwa kuibua wagonjwa wapya kupitia wale waliokuwa wameyapata maradhi hayo pamoja na kushirikiana na waganga wa jadi, maduka ya dawa muhimu ambapo wagonjwa wengi huanzia kwao.
Mkutano huo wa siku tatu umelenga pia kutathimini hali ya magonjwa hayo kwa mwaka mmoja uliopita pamoja na kupanga malengo ya kuboresha na kuhakikisha mipango iliyowekwa inafikia malengo ya kupunguza magonjwa hayo.
chanzo:mwananchidigital
No comments:
Post a Comment