Hakimu anayesikiliza kesi ya Jinai namba 12/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake 83 ametupilia mbali maombi ya upande wa utetezi ya kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwa kile alichodai hayana mashiko kisheria.
Katika maombi yaliyowasilishwa Jumatano Novemba 9, 2022 na jopo la mawakili wa utetezi, washtakiwa walimtaka hakimu ajiondoe kwa kile walichotaja kuwa ni kukosa imani naye baada ya kuonekana akichana karatasi wakati kesi ikiendelea bila kueleza nini kinachochanwa na nini kitaandikwa.
Pia, washtakiwa hao walidai hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Clescensia Mushi hakuwasomea ushahidi waliyotoa mashahidi watatu katika kesi ndogo iliyoibuka ndani ya kesi ya msingi kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 210 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) ya mwaka 2019.
Akisoma maamuzi kuhusu maombi ya washtakiwa kumtaka ajitoe kwenye kesi hiyo, Hakimu, Mushi amesema baada ya kupitia Sheria, Miongozo na Kanuni za mahakama amejiridhisha kuwa hayana mashiko wala hayakidhi kumfanya ajitoe kusikiliza kesi hiyo.
Chanzo:mwananchidigital
No comments:
Post a Comment