SERIKALI kupitia Mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) imesema inatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya malipo kwa watumishi wa Umma 9000 waliondolewa kazini kwa sababu ya vyeti feki.
Hatua hiyo imekuja kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutaka watumishi hao walipwe michango yao waliyochangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii huku akisema utekelezaji huo uanze Novemba Mosi, 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea Kashimba amesema hayo leo Jijini hapa wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu shughuli za utekelezaji wa Mfuko huo na kueleza kuwa Mfuko huo umejipanga kuwapa kipaumbele wanachama hao mara watakapo pokea madai yao kutoka kwa waajiri.
Amesema ili walengwa hao wapate stahiki zao wanapaswa kufuata taratibu za uajiri ammbapo wanatakiwa kuwasilisha madai yao Kwa waajiri Ili kupeleka vielelezo kwenye Mfuko huo kisha marejesho ya michango Yao kuanza kufanyika kuanzia tarehe moja, Novemba, na kusisitiza kuwa wangependa jambo hilo likamilike ndani ya muda mfupi.
"Ili kuwezesha malipo hayo kufanyika mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri na kuchukua nyaraka zote muhimu ambazo zinatakiwa na sisi PSSSF tutakuwa na jukumu Moja tu la kutekeleza agizo la Rais Samia,"amesema.
Pamoja na hayo CPA Kashimba ameeleza kuwa Mfuko huo unatambua Moja ya changamoto kubwa kwenye jamii ni uelewa mdogo kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii hivyo PSSSF imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wanachama wake Ili kuhakikisha sekta hiyo inafanikiwa .
Amesema ili jitihada za kuhakikisha lengo la kutoa huduma bora linatimia,Mfuko unaendelea kutekeleza mambo mbalimbali yanayolenga kurahisisha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na mtandao wa Ofisi za Mfuko ambapo una Ofisi Kila Mkoa na baadhi ya Wilaya Kwa lengo la kuwa karibu na wanachama.
"Mfuko una kituo cha kupiga simu bure kwa ajiri ya wanachama ambapo huduma hutolewa hadi saa mbili usiku ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa masuala ya yanayohusu huduma mbalimbali za uanachama,"amesema CPA Kashimba.
Akieleza matarajio ya baadae , amesema wanatarajia kuongeza vituo vya uhakiki Katika halmashauri mbalimbali na kuanzisha utaratibu wa kujihakiki kupitia simu janja na kusaidia Kila taarifa ya mwanachama iwe kwenye mfumo.
"Matarajio mengine ni kuhakikisha mifumo ya PSSSF inasomana na mifumo mingine kutoka Taasisi za Umma zinazotoa huduma,kurahisisha uandikishaji wanachama na uletaji wa madai kupitia mtandao na kutumia mifumo mipya ya Tehama kulingana na mahitaji ya Mfuko,"amesema
Mfuko wa PSSSF ni matokeo ya kuifuta mifuko ya hifadhi ya jamii ya LAPF,PSPF,GEPF,PPF na kuanzisha Mfuko wa huo ambapo waliokuwa wanachama wa mifuko hiyo walihamishiwa kwenye Mfuko wa PSSSF na wataendele kuwa wanachama na kuchangia .
No comments:
Post a Comment