Hamimu Yunusu, mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga ambaye mwaka 2018 alihukumiwa kifungo cha miaka 34 jela kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne na kumwambukiza Ukimwi kwa makusudi, ameachiwa huru.
Hukumu ya Yunusu ilijumuisha kifungo cha miaka 30 kwa kubaka na miaka minne kwa kumwambukiza Ukimwi mwanafunzi huyo kwa makusudi. Hata hivyo, Ijumaa ya Novemba 4 mwaka huu, milango ya matumaini ilifunguka kwake baada ya Mahakama ya Rufani kumwachia huru.
Yunusu amerudi uraiani baada ya jopo la majaji watatu ambao ni Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Panterine Kente kuzikubali hoja za rufaa aliyoiwasilisha kupinga adhabu hiyo baada ya kubaini dosari za kisheria katika uchukuaji ushahidi kutoka kwa mtoto huyo na wenzake.
Hata hivyo, baadhi ya mawakili na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa na maoni tofauti juu ya hukumu za kesi za aina hiyo na nyingine kufutwa au kuagiza kusikilizwa upya kutokana na dosari za kisheria za baadhi ya majaji au mahakimu.
Baadhi ya mawakili hao wamesema ni wajibu wa maofisa wa mahakama ambao ni mawakili wa mashitaka na utetezi, kumkumbusha jaji au hakimu pale anapopitiwa katika uchukuaji wa taarifa za mwenendo wa kesi kwa kuwa nao ni binadamu.
No comments:
Post a Comment