Waraghbishi wa kundi wakiwasilisha maoni ya changamoto za Uraghbishi kuhusishwa na masuala ya kisiasa.
Kundi la Waraghbishi wakijitambulisha baada ya kuwasilisha hoja za utatuzi na uboreshaji wa kazi za Uraghbishi.
-----------------------------------------------
WARAGHBISHI ambao ni wananchi wachochea maendeleo katika jamii wametakiwa kutokujihusisha na itikadi ya vyama vya kisiasa ili kutimiza lengo la shughuli za Uraghbishi ambazo zimekuwa zikitumika kuwakutanisha wananchi na serikali ili kuleta maendeleo.
NA PASCHAL MALULU-HUHESO DIGITAL- DAR ES SALAAM
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 07, 2022 na wawakilishi wa vikundi vya wajumbe waliohudhuria Tamasha la Waraghbishi kwa lengo la kupata maoni ya namna ya uboreshaji wa ushirikiano na viongozi wa ngazi za juu, katika kilele cha Tamasha hilo lililokuwa likifanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC Hotel Jijini Dar es salaam.
Hatua hiyo iliibuka baada ya Waraghbishi hao kutoa changamoto zao ikiwemo ya kukosa ushirikiano kwenye maeneo yao kutokana na kubainika kuibua au kuchokonoa kero na changamoto zinagusa maslahi ya viongozi mbalimbali wa ngazi ya juu hivyo kuonekana kama Waraghbishi wanataka madaraka hasa ya kisiasa.
Wamesema katika vipaumbele vya serikali na bajeti zake kumekuwa na miradi ya maendeleo inayopelekwa kwenye maeneo yao lakini wao kama Waraghbishi wanaisaidia serikali kuifikishia mahitaji ya wananchi kwani kumekuwa miradi inayopelekwa wakazi wa eneo husika wanauhitaji wa mradi mwingine.
Katika mjadala huo wamebainisha kuwa wananchi wanaotumika kuibua mahitaji ya wananchi au kero na changamoto wanaonekana kutumika kisiasa hali inayochangia kuonekana wabaya na kukosa maelewano hivyo wameliomba shirika la TWAWEZA ambalo linashughulikia mradi huo kuongeza nguvu ya kuwajengea uwezo na elimu viongozi wote wa kiserikali na kisiasa kutoa ushirikiano kwa Waraghbishi.
"Tumekuwa tunaonekana tunataka madaraka, au kiongozi fulani tunataka ufukuzwe kwahiyo hii imekuwa inatupa changamoto kuwa wengine mpaka tunaitwa na kuhojiwa uhalali wetu wa kufanya kazi hii ya kuibua mahitaji ya wananchi na kuwashirikisha ili kushiriki".
Wakitoa shuhuda mbalimbali Waraghbishi wamedai kuwa wamekuwa wakiitwa Wanaharakati kutokana na kuwa wachokonozi wa kero ambazo kwa hali ya kawaida zilipaswa kufanywa na Diwani, Mbunge wa eneo husika hivyo wanapowafuata viongozi hao wanakosa ushiriano wao kwani wanapokelewa kwa mtazamo tofauti ya kuonekana wanawadhoofisha kwa wananchi ili kujitwalia madaraka.
Akijibu hoja za Waraghbishi za kukosa ushirikiano Richard Temu afisa Ushiriki kutoka Shirika la TWAWEZA amesema wao wamekuwa wakiwapatia elimu viongozi mbalimbali na kuwatambulisha wananchi Waraghbishi wote kwenye mikoa yote pamoja na halmashauri ili kuwatambu ili kuwapatia ushirikiano.
Amesema mradi wa Uraghbishi unafanyika katika mikoa nane ya Dar es salaam, Tanga, Simiyu, Shinyanga, Geita, Lindi, Mtwara na Kigoma hivyo kwenye maeneo hayo kuna baadhi ya maendeleo yamepatikana ikiwemo Elimu, Afya, miundombinu ya Barabara huku washiriki wakubwa wakiwa ni wananchi.
Uraghbishi unatajwa kuwa ni shughuli ambayo inajishughulisha na wananchi kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo badala ya kuisubiri serikali huku mradi husika wananchi na wakazi wa kijiji au Mtaa husika wakishirikishwa wanao uwezo wa kuitatua changamoto hiyo.
Aidha kazi ya Uraghbishi imebainika ni wananchi wachochea maendeleo kwa haraka na kwa muda mfupi katika utatuzi wa changamoto.
Tamasha la Waraghbishi limefungwa hii leo Oktoba 07, 2022 ambalo lilianza Oktoba 05, 2022 ikiwa limefanyika kwa muda wa siku tatu kwa majadiliano ya mada mbalimbali za uboreshaji wa Uraghbishi na ushirikiano wa Waraghbishi na Vyombo vya habari nchini ili kuifikia jamii na lilikuwa limeandaliwa na Shirika la TWAWEZA TANZANIA na kushirikisha jumla ya washiriki 180.
PICHA ZOTE NA ERICK FELINO-HUHESO DIGITAL-DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment