SHIRIKA la Matumaini na Maendeleo Kanyigo(SMK),limezindua kiwilaya,mradi wa Ufuatiliaji wa Uwajibikaji katika Jamii (Social Accountability Monitoring),utakaoendeshwa katika kata nane zilizoko tarafa ya Kiziba, ambazo ni Kashenye,Kanyigo,Bwanjai na Ishozi.
Na Mutayoba Arbogast Huheso Blog, Bukoba
Baadhi ya viongozi wa shirika na washiriki(wa tatu kutoka kushoto ni Makamu mwenyekiti wa Halmashsuri ya Missenyi,Regina Rwamuganga)
Kata nyingine zitakazohusika na mradi huo ni Gera,Bugandika,Buyango na Ruzinga,huku kata mbili za Ishunju na Kitobo hazikufikiwa na mradi huu kutokana na ufinyu wa bajeti.
Akifafanua juu ya mradi huu kwa wajumbe walioalikwa ambao ni kutoka Halmashauri ya wilaya ya Missenyi,madiwani na maafisa kilimo kutoka kata husika ,Mratibu wa SMK, Frederick Mujwahuzi,amesema mradi unalenga kukuza ushiriki wa wananchi katika kufuatilia mchakato ya kiutendaji na utoaji wa huduma ndani ya jamii.
Kwamba dhana ya Uwajibikaji inazingatia upatikanaji wa haki za msingi za raia wote katika kusimamia na kutumia raslimali za umma kwa manufaa yao.
Kila kata itatoa watu watano kwa kuzingatia makundi yote ikiwemo wenye ulemavu,vijana na wanawake,ambao watapatiwa semina ya siku tatu kuhusu Ufuatiliaji na kisha kuingia kazini ambapo watafuatilia na kudodosa mambo anuwai kuhusu kilimo kama ikama ya maafisa ugani,upatikanaji wa pembejeo,uwajibikaji wa wananchi katika kilimo hususan vijana nk.
Mwenyekiti wa shirika hilo,Samweli Bashweka,kupitia madiwani,amezihimiza Kamati za maendeleo za kata(WDCs),jkuwachuja vizuri wanaoomba nafasi katika Kamati za Ufuatiliaji baada ya kuwa wamejaza fomu ili kupata watu sahihi.
Diwani wa kata ya Gera,Henry Bitegeko kwa niaba ya washiriki amesema wameupokea mradi huo kwa furaha kwani utaleta mabadiliko katika kilimo ambavyo ndio uti wa mgongo wa taifa.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Missenyi,Regina Rwamuganga,amelishukuru shirika hilo kwa kuibua miradi mbalimbali,na akalihimiza utekelezaji kadri ya mpango kazi ili kuleta ufanisi.
Shirika hilo limepata ufadhili wa zaidi ya sh. milioni 53 kutoka Foundation for Civil Society,ili kuleta mabadiliko ya tija katika sekta ya kilimo.
Samweli Bashweka,Mwenyekiti wa SMK,akitoa neno kwa washiriki
Baadhi ya washiriki katika kikao cha kuutambulisha mradi
No comments:
Post a Comment