Jumuiya ya umoja wa vijana wa kiislam Tanzania (TAMSIYA),Mkoa Shinyanga wameaswa kutafuta elimu ya dunia na akhera ili kuondokana na imani potofu za bahati nasibu maarufu kama kubeti ili kuwepo na wasomi sambamba na wataalamu wazuri katika taifa.
NA HALIMA KHOYA-HUHESO DIGITAL SHINYANGA
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga,Jomary Satura,Ambaye alikuwa ni Mgeni rasmi katika mahafali ya TAMSIYA Mkoani humo yaliyofanyika jana Oktoba 23 mwaka huu katika ukumbi wa CCM Mkoa iliyojumuisha shule 13 kati ya shule 28 zilizopo Mkoani humo.
Mkurugenzi Satura, amebainisha kuwepo kwa vijana wasiotaka kusoma huku wakitegemea bahati nasibu maarufu kama kubeti ambapo vijana hao wanaharibika na kudumaa kiakili hali inayopelekea kuwepo kwa uchache wa wataalamu na wasomi hapa nchini.
Vile vile Satura amesema kuwa licha ya kuwepo kwa wanafunzi wanao faulu katika masomo yao bado kumekuwa na changamoto kubwa wanayopitia wazazi wanapowasomesha vijana wao hali inayoumiza wazazi na walezi wengi pale vijana wao wanapofeli katika masomo yao.
"Aya Ya kwanza kumshukia mtume ilikuwa ni "Iqra Bismi rabika ladhi khalak,Soma kwa jina la Mola wako"Lakini sasa vijana wengi hamtaki kusoma alafu unadhani maisha utayapata kwa kubeti,kijana unajikita kwenye kubeti,mnasubiria zari liwaangukie akati Mwenyezi Mungu anasema tusome ili kufanikiwa katika mambo yetu"Amesema Satura.
"Naomba niwasihi ili kwenda katika mafanikio yenu hakuna njia nyingine mbadala na nyepesi,hata ukitaka kuwa mjasiriamali lazima uwe na maarifa,na jambo.lolote unalotaka kulifanya msingi wake ni maarifa"Ameongeza Satura.
"Niwasihi wazazi wenzangu watoto hawa hawajui tunawategemea kiasi gani,hawajui kwamba ipo siku mtazeeka na mtawahitaji wao waje kuwasaidia,hawajui mnawasomesha kwa kukopa kwenye vikoba hivyo basi wazazi pale mnapopata nafasi muwaeleze kwamba mnawasomesha katika mazingira magumu"Ameongeza Satura.
Kwa upande wake Katibu wa idara ya Elimu TAMSIYA Mkoa Shinyanga,Jamal Faki,amewaasa watahiniwa hao kufanya maandalizi kwa kusoma na kufanya mitihani mbali mbali ili kuepuka changamoto ya kusoma kwa muda mrefu ifikapo siku ya kuingia katika chumba cha mtihani hali itakayosababisha kupata homa ya mtihani (Examination fever) kwa wanafunzi wasio na maandalizi yakutosha.
Nao baadhi ya wahitimu wa kidato cha nne wamebainisha kujiamini kwa kukabiliana na Mtihani wa Taifa kwa kuwa na maandalizi yaliyojitosheleza huku wakimtoa hofu Mkurugenzi kuwa watasoma elimu zote (Dunia na Akhera) ili kuleta maendeleo mazuri na ufaulu uliokuwa bora hali itakayopelekea kuwepo na kizazi chenye maarifa katika jamii.
No comments:
Post a Comment