RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuiga mfano wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere,Rais wa kwanza wa Tanzania(wakati ule Tanganyika),kwa uadilifu wake kwa kuikataa rushwa, uzembe na ubadhirifu wa mali za umma.
Kiongozi wa mbio za mwenge,Sahili Nyanzabara Geraruma,akimkabidhi Rais Samia,ripoti ya ukaguzi wa miradi iliyotembelewa na mwenge 2022
Na Mutayoba Arbogast,Bukoba
Rais Samia ametoa kauli hiyo jana mjini Bukoba,mkoani Kagera, katika maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge 2022,yaliyokwenda sambamba na kumbukumbu ya kifo cha muasisi wa taifa hili,mwl Julius Kambarage Nyerere aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999.
"Hakuna asiyefahamu kwamba rushwa ni adui wa haki, awamu zote za uongozi zilizopita zimepambana na vitendo vya rushwa nguvu kubwa.Kwa mujibu wa toleo la Shirika la Kimataifa la Uwazi la Januari,2022, Nchi yetu ni miongoni mwa Nchi sita zilizopiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika. Katika jitihada za kuendelea kupiga vita maadui njaa, ujinga, maradhi na umasikini, Serikali zetu mbili zimeendelea kutenga fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.Inasikitisha kuona kwamba kuna watu wasiojali wala kuhurumia wananchi na kuwapa miradi Wakandarasi wasio na uwezo,watu waliotawaliwa na rushwa, wezi na wengine ni wazembe wanaosababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo",amesema Rais.
Ameyasema hayo baada ya kupokea ripoti ya kiongozi wa mbio za mwenge 2022 Sahili Nyanzabara Geraruma,kuwa mwenge umekataa kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 65 kutoka Halmashauri 43 yenye thamani ya Shilingi bilioni 12 iliyobainika kuwa na dosari ikiwemo ujenzi chini ya kiwango, rushwa,uzembe na ubadhirifu na ukiukwaji wa mikataba.
Jumla ya miradi iliyotembelewa na mwenge ni 1,263 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 650.
Rais Samia amewaelekeza TAKUKURU na ZAECA(Zanzibar) kufanya uchunguzi na kuchukuwa hatua stahiki kwa wote waliobainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma,lakini akiagiza wao wajifanyie tathmini kwanza kama wako safi,akinukuu maneno ya Biblia kuwa,'Kabla hujatoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako,toa kwanza boriti kwenye jicho lako'
Awali amehudhuria Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Bukoba,misa ambayo imeongozwa na Askofu Methodius Kilaini, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bukoba,kumuombea hayati mwalimu Nyerere,ambaye pia alitangazwa na Baba Mtakatifu Benedicto wa 16, kuwa ni Mwenye Heri,ikiwa ni mwanzo wa mchakato wa kutangaza kuwa Mtakatifu,na akaruhusu maoni kumhusu.
Aidha,Rais amewashukuru vijana kushiriki Wiki yao ya Vijana, na kuonesha kuwa wapo tayari kushiriki katika harakati za kunyanyua uchumi wa taifa lao kupitia ubunifu na huduma mbalimbali wanazotoa.
Ameonya juu ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya kuwa ni tatizo sugu, hadi kufikia Disemba 2021, wagonjwa 189,000 walipatiwa tiba ya uraibu na magonjwa yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya na kuwa tatizo hilo linagharimu fedha nyingi katika kutibu wagonjwa, pamoja na kupoteza nguvu kazi kubwa ya taifa.
Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dr Phillip Isidor Mpango baada ya kuhudhuria Misa Takatifu.Kulia kwa Rais ni Msimamizi wa Kitume,Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu Methodius Kilaini
Sehemu ya vijana wakiteta jambo katika maadhimisho hayo.
Sehemu ya umati uliofurika na kutapika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kilele cha mbio za mwenge 2022
No comments:
Post a Comment