Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza milango iliyowekwa kwenye hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ing'olewe na badala yake iwekwe yenye hadhi.
Waziri Mkuu akikagua milango
Maagizo hayo ameyatoa hii leo Oktoba 18, 2022, wakati alipokagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo na kusema serikali haiwezi kukaa kimya huku baadhi ya watumishi wakifanya vitendo vya hovyo.
"Nimekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya lakini sijaridhishwa na hali ya ujenzi, nimeagiza milango yenye hitilafu yote ing'olewe na iwekwe yenye hadhi ya hospitali ya wilaya, iweje imeacha nafasi juu hadi vidole vinapita? mtu akifunga mlango wewe uliyeko nje unaona ndani, hii haikubaliki, RC simamieni milango hiyo itolewe, na ije yenye hadhi," amesema Waziri Mkuu
"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta shilingi bilioni 7 za ujenzi wa hospitali hii, fedha hizi za ujenzi ni lazima wananchi waone thamani ya fedha zao, siwezi kukubaliana na utendaji wa hovyo fedha ziko hapa tangu Aprili, ni kwanini hadi sasa majengo yapo kwenye lenta? huu ni ubabaishaji," ameongeza Waziri Mkuu
Mapema akikagua ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya milango imepishana urefu licha ya kuwa inapaswa ikutane ili kitasa kiweze kufunga, mingine ilikuwa inagoma kufunga, inarudi nyuma na kubakia wazi na pia aligusa mlango na kukuta varnish bado haijauka.
CHANZO:EATV
No comments:
Post a Comment